Yanga Yasajili Straika Mpya wa Maana

Yanga Yasaka Saini Ya Straika Wa Kagera
ZIKIWA zimebaki siku moja kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili hapa nchini, uongozi wa Yanga unajipanga vilivyo kuhakikisha unakiimarisha kikosi chake ili kiweze kufanya vizuri katika mechi zake zijazo za Ligi Kuu Bara lakini pia katika michuano ya kimataifa.

Uongozi unahitaji kusajili wachezaji wanne katika dirisha hili dogo la usajili kwa ajili ya kuziba upungufu uliojitokeza katika kikosi hicho tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu katika nafasi ya ulinzi, kiungo pamoja na ushambuliaji. Na tayari mazungumzo na straika mmoja wa Kagera Sugar yanaendelea.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Jumatatu limezipata zimedai kuwa mpaka sasa uongozi huo umeishaanza mazungumzo
na baadhi ya wachezaji ambao inawahitaji akiwemo Mtogo Vincent Bossou ambaye ilimuacha baada ya kumalizika kwa msimu uliopita lakini pia kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohamed Issa ‘Banka’.

Ukiachana na wachezaji hao ambao taarifa zao zimekuwa zikisemwa sana hivi karibuni pia uongozi huo unadaiwa kuwa katika mazungumzo na Straika wa Kagera Sugar, Jafar Kibaya ambaye ni kati ya washambuliaji mahiri hapa nchini.

Mshambuliaji huyo ndiye aliyeivuruga ngome ya Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu alipoifungia timu yake bao moja wakati Yanga iliposhinda 2-1 na kuwazidi ujanja mabeki wawili matata wa timu hiyo, Kelvin Yondani na Andrew Vicent Dante ambao imekuwa adimu sana wao kufungwa msimu huu.

Akizungumza na Championi Jumatatu, mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye aliomba kutotajwa jina lake, alisema uongozi huo unajipanga kuhakikisha unamsajili Kibaya ili kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji ambayo tangu kuanza kwa ligi kuu imekuwa ikiwategemea Ibrahim Ajibu pamoja na Mzambia, Obrey Chirwa.

“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo tumeona ni bora tupambane kuhakikisha tunamsajili Kibaya kwa ajili ya kuja kusaidiana na wachezaji hao kwani Donald Ngoma na Amissi Tambwe kwa sasa siyo wachezaji wa kuwategemea sana.

“Muda mwingi wamekuwa nje ya uwanja, jambo ambalo linatufanya tuwe na wakati mgumu pindi wanapoumia, kwa hiyo Kibaya anatufaa na tayari kocha ametuambia tuhakikishe tunamsajili kwani alimuona tulipocheza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba na alitusumbua sana,” alisema kiongozi huyo.

Katika mchezo huo dhidi ya Yanga, Kibaya ndiye aliyefunga bao pekee la Kagera ambapo Yanga ilishinda 1-2.
Alipoulizwa suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema: “Muda wa usajili bado haujafika kwa hiyo kwa sasa siwezi kuzungumzia hilo, tusubiri kwanza mpaka utakapofika muda huo.”

Hata hivyo, Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein alipoulizwa kama wapo tayari kumuachia mchezaji huyo ajiunge na Yanga alisema: “Waje tuzungumze kama watakuwa tayari kutupatia fedha ambayo tutawaambia haina shida kwani Kibaya bado ana mkataba wa miaka miwili na sisi.

“Tumemsajili msimu huu akitokea Mtibwa Sugar kwa hiyo wakikubali kutupatia fedha tutakayowaambia basi tutawapatia.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad