Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imeipiga faini ya sh. 500,000 (laki tano) mabingwa watetezi klabu ya Yanga baada ya kitendo cha mashabiki wake kurusha uwanjani chupa zinazosadikiwa kuwa na mikojo katika mchezo wao dhidi ya watani zao wa jadi Simba SC.
Kamati hiyo imeikuta klabu ya Yanga na hatia baada ya kupitia ripoti za michezo yote ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Yanga SC inakabiliwa na hadhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 42(1) kuhusu udhibiti wa klabu.
Katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara namba 58, mabingwa watetezi klabu ya Yanga ilishuka dimbani Oktoba 28 kukabiliana na Simba SC Uwanja wa Uhuru.
Katika mchezo huo wa watani wa jadi uliamuliwa kwa sare ya1-1, wakati Simba SC ikiwa ya kwanza kujipatia goli kupitia kwa Shiza Ramadhani Kichuya huku wenyeji Yanga wakisawazisha bao hilo kupitia Obrey Chirwa.