Anaandika Mbunge wa Kigoma Zitto Kabwe.
Jambo moja linanisumbua sana. Nisaidieni tafadhali
Inawezekanaje Serikali ikasaini mkataba wa shilingi Trilioni 7 kujenga Reli bila kuweka vifungu vya kufungamanisha na sekta nyengine nchini? Yani kweli hata misumari ( screws) nchi hii haiwezi kutengeneza mpaka iagizwe kutoka Uturuki? Yani hata kampuni ya kuchimba kokoto itoke Uturuki? Hivi Viwanda vya Chuma nchini vinafanya kazi gani sasa? CTI, TPSF nielezeni hili, hamuwezi kuzalisha kitu chochote kulisha ujenzi wa Reli ya Kati ya SGR? Katika BOQ ya Mradi wa SGR, hamna muwezalo? Serikali iliwapa BOQ mkashindwa? Ukiwauliza watu wa Wizara hawana majibu, wanasema Mkataba ali negotiate Rais mwenyewe. Inawezekana kweli? Siwezi kumwuliza Rais. Anasema sisi kazi yetu kukosoa tu. Amekasirika. Siwezi kumwuliza mtu aliyekasirika, tena Amiri Jeshi Mkuu.
Wakati wa Mdororo wa Uchumi Asia mwaka 1997-1998 Waziri Mkuu wa Malaysia Tun Mahathir Mohammed alifanya miradi mikubwa sana ikiwemo kujenga Mji Mpya, barabara kubwa na Jengo la Petronas. Kwanini? Ili kuingiza fedha kwenye uchumi na kuchochea shughuli nyengine za uchumi na kukuza mahitaji ( aggregate demand). Malaysia ikawa nchi ya kwanza kuibuka kutoka Asian Financial Crisis.
Sisi Watawala wetu wamekwenda madarasa tofauti na kusoma vitabu tofauti vya Uchumi? Unajenga Reli kwa pesa yako ( inavyodaiwa), kwa hiyo unakusanya kodi kutoka kwa watu wako, unanunua US$, unamlipa Mkandarasi. Mkandarasi ananunua kila kitu kutoka nchini kwao Uturuki, mataruma ya Reli, Chuma, Screws na Misumari na hata mchimba kokoto Mturuki. Kwenye uchumi hii inaitwa leakages. Uchumi wetu unahitaji more inflows.
Unajengaje Reli kwa kutumia Chuma kutoka nje the wakati una hazina ya chuma Ludewa? Unamwaga TZS 7 Trilioni bila kuhakikisha offsetting? Natamani kuiona hiyo BOQ ya Reli ya Kati.
Hili linanisumbua sana. Siamini kuwa watawala waliokwenda shule na wenye uzoefu Serikalini hawakuona faida kubwa ya offsets. Baraza la Mawaziri limejaa PHDs, kweli wameshindwa kuona hili? Fedha zetu wenyewe tunatengeneza ajira nje? Kwamba sisi tuwe vibarua tu na wagonga reli? Trilioni 7 zingechochea sana uchumi ( multipliers).
Tunaambiwa sisi tupo negative mno. Hebu watetezi wa Serikali, mnaojua kuitafsiri Serikali, nisaidieni. Hili mnaona lipo sawa?