Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Marekani Hope Solo, mwenye umri wa miaka 36 ametangaza rasmi kuwania nafasi ya Rais wa shirikisho la soka nchini humo (USSF) mwaka 2018.
Hope Solo ameweka wazi mpango wake huo wa kuwania nafasi hiyo ya kuongoza soka nchini Marekani huku akieleza moja ya sababu kubwa ni kuporomoka kwa kiwango cha timu za taifa za soka za wanawake na wanaume.
Rais wa USSF wa sasa Sunil Gulati ametangaza kutogombea tena nafasi hiyo akitaja sababu kuwa ni kuwajibika baada ya timu ya wanaume kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi. Gulati mwenye umri wa miaka 58 amekuwa rais wa USFF tangu 2006.
"Nilipokuwa msichana mdogo, kitu pekee nilichotaka ni kucheza soka na kuichezea timu yangu ya taifa katika ngazi zote na nimefanikiwa kufanya hivyo, kinachofanya ni kulitendea haki taifa langu na kurejesha heshima ya soka kwa kuwa rais wa USSF”, amesema Hope Solo.
Hope ameongeza kuwa katika muda wote ambao amekuwa mchezaji na hata baada ya kustaafu amekuwa akijifunza kutoka kwa marais wengine duniani hivyo ana uhakika amepata uzoefu wa kutosha kuweza kuisaidia nchi yake.