Kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na kunajisi mwaka 2017, yamewaibua viongozi wa dini na wanaharakati, wakisema jamii inachangia kwa sehemu kubwa huku wakitaka sheria na adhabu kali zitolewe kwa wahusika watakaobainika kutenda makosa hayo.
Taarifa ya usalama wa nchi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Desemba 20 na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz inaonyesha kuwa matukio hayo yameongezeka kutoka 6,985 mwaka jana hadi 7,460 mwaka huu.
Alisema makosa dhidi ya binadamu, yanayojumuisha mauaji, kubaka, kulawati, wizi wa watoto, kutupa watoto, kunajisi pamoja na usafirishaji wa binadamu, yameongezeka kutoka 11,513 mwaka jana hadi 11,620 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la makosa 107.
Hata hivyo, DCI Boaz alibainisha kuwa makosa makubwa ya jinai yamepungua kutoka 68,204 mwaka jana hadi 61,794 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka huu.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu takwimu za matukio, Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki Bukoba mkoani Kagera, Methodius Kilaini alisema inasikitisha kuona bado kuna watu wanaendelea na vitendo vya ubakaji na kunajisi licha ya kuwepo adhabu kali.
“Sisi viongozi wa dini, kisiasa na jamii tunapaswa kukemea vitendo hivi ambavyo mara nyingi vinafanywa na watu wa karibu. Lakini kunaporipotiwa watu kutenda makosa haya adhabu kali zichukuliwe kwa haraka ili iwe funzo,” alisema Askofu Kilaini na kuongeza, “Mtoto ni malaika, unapoona mtu kamnajisi halafu unamfumbia macho kisa ni ndugu yako na mnakaa ndani ili kumaliza suala hili pembeni ni hatari, mtu anapomnajisi mtoto huyo ni shetani, hivyo jamii tukemee matendo haya kwa nguvu zote.”
Askofu Kilaini aliungwa mkono na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum akisema, “Ni jambo la kusikitisha. Elimu kwa jamii juu ya madhara haya ni ndogo, adhabu ni ndogo ila kubwa ni mmomonyoko wa maadili.”
“Mavazi ya baadhi ya watoto wa kike nayo yanachangia, uhuru wa watoto kuachwa wanacheza na wavulana hadi kufikia kumbaka, hivyo sheria iwe kali kwa atakayebainika lakini somo la maadili liongezwe nguvu kwani hadi mtu anafanya hayo anakuwa hana hofu ya Mungu.”
Katika taarifa yake, DCI Boaz anasema makosa dhidi ya maadili ya jamii nayo yalipungua kutoka 20,000 mwaka jana hadi kufikia 18,971 mwaka huu ikiwa ni sawa na pungufu ya makosa 1,029.
Akichambua taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Eda Sanga alisema ongezeko hilo limechangiwa na elimu inayotolewa ambayo imesaidia waathirika kutoa taarifa huku akiomba ushirikiano wa pamoja kumaliza tatizo hilo.
“Zamani watu walikuwa hawatoi taarifa, wakikutwa na tatizo wanakaa kimya lakini unapomuelimisha mtu anaelewa na anatoa taarifa lakini pia ukiielimisha jamii kuhusu madhara haya, inasaidia kupunguza tatizo,” alisema Sanga.
Sanga alisema kama kasi hiyo ya matukio ikiendelea hivyo mwaka 2018, siku za usoni kutakuwa na Taifa lisilokuwa na maadili hivyo viongozi wa dini, Serikali na jamii wanapaswa kukemea hili kwa nguvu zote na vitendo vyao vionekane kupinga hili.
Katibu mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT), Leonard Mtaita alisema “Na mimi nimesikia lakini nanichoweza kusema ni siku za mwisho zimekaribia. Watu watatenda maovu na tutayaona mengi, kikubwa wamrudie Mungu na kuacha maovu.”