BOT Yaagizwa Kuzifutia Leseni Benki Zisizokidhi Vigezo Kufutwa

BOT Yaagizwa Kuzifutia Leseni Benki Zisizokidhi Vigezo Kufutwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania BOT kuzifutia leseni benki zote za biashara pamoja na benki za wananchi zitakazoshindwa kukidhi vigezo vya kuendesha shughuli za kibenki nchini.

Ametoa agizo hilo mjini Dodoma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua Mkutano Maalum wa Wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT).

“kwa taarifa niliyonayo hadi sasa baadhi ya benki hazijatimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa kutosha, hali ambayo haiwezi kuachwa iendelea hata kidogo, kwani haiimarishi sekta ya fedha na haiwasaidii wananchi kuendelea kiuchumi” alisema Waziri Kassim Majaliwa katika hotuba hiyo.

Alisema Benki Kuu ilitoa muda hadi mwishoni mwa Desemba 2017, benki za wananchi ziweze kuongeza mtaji na kwamba muda huo hautaongezwa na wala Serikali haitatoa mtaji kwa benki hizo.

“Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania haitasita kuifungia benki yoyote na kufuta leseni yake ya biashara pindi itakapobaini inavunja sheria, ikiwa ni pamoja na kuwa na upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi ambao unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na amana za wateja kama tulivyofanya kwa Mbinga Community Bank PLC kuanzia tarehe 12/5/2017” alisema Dkt. Mpango kwa niaba ya Waziri Mkuu.

Maagizo hayo yamekuja siku moja baada ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango wakati akifungua tawi kuu la Benki ya CRDB mjini Dodoma, kuhakikisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania-BOT, inazifuta benki zote zinazoshindwa kujiendesha kibiashara hata kama zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Alisema Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha benki za wananchi zinaimarika zikiwemo kuruhusiwa kuanzisha mifumo ya ushirikiano katika Nyanja ya Mfumo wa Mawasiliano na Habari (ICT), Idara za Ukaguzi wa Ndani (Internal Audit Services), kupunguza wingi wa idara na kuwa na idara tatu (3) tu muhimu, kuruhusiwa kuungana (Federation), ambazo zitapunguza gharama za uendeshaji wa benki za wananchi na kuleta ufanisi katika kutoa huduma.

“Napenda kusisitiza kuwa sekta ya benki ni muhimu sana kwa uhai na ukuaji wa uchumi kama ilivyo damu kwa mwili wa binadamu na kutokana na umuhimu wake huo, sekta hii ni kati ya sekta chache zinazosimamiwa kwa karibu sana ili kulinda amana za wateja pamoja na kuhakikisha uhimilivu wa mfumo mzima wa sekta ya fedha na mwenendo wa uchumi wa Taifa” aliongeza Dkt. Mpango

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT) Bw. Rukwaro Senkoro, alisema hadi kufikia Juni, 2017, Benki za Wananchi nchini zilikuwa na wateja zaidi ya milioni 1.4, wateja wa vikundi zaidi ya 10,000, Matawi 12, Vituo 59, na wanahisa 66,492.

“Benki hizo zina amana zenye thamani ya shs bilioni 74.2, zimetoa mikopo ya sh. bilioni 56.8, na jumla ya mali zenye thamani ya shs. bilioni 92.3” Alisema Bw. Senkoro

Hata hivyo, kutokana na Utafiti wa Matumizi ya Huduma za Kifedha uliofanyika mwaka 2017 umebaini kuwa asilimia 28 ya wananchi bado hawapati huduma za kifedha hapa nchini hususan vijijini na kutaja changamoto ya ukosefu wa mitaji ya benki hizo kukwaza sekta hiyo.

Dhana kuu ya mkutano huo wa COBAT uliowashirikisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni “Mitaji na Mpango wa Kuziunganisha Benki za Wananchi Tanzania”, ambayo ni dhana mpya.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Swadakta.. Mh Kassim Majaliwa.
    Swadakta.. Baba JPJM
    Swakta Mh Mipango.

    Nnnasema Dodoma ni Tulivu na Ina Pumzisha vichwa na Fikra.. Maamuzi na Maagizo yake ni Mazito.

    Mnakaribishwa sana Dodoma na Tuendelee kuifanyia kazi nchi yetu kutokea Dodoma.. Ninayo imani Tanzania yetu mpya is achievable in even shorter than expected time.
    Miongozo toka Dodoma na Ufatiliaji ni Nchi nzima.
    Napendekeza tuunde wizara ya Ufatiliaji ambayo itakuwa haina kikomo katika utendaji na ufatiliaji
    ambayo itakuwa chini ya Ofisi ya Waziri mkuu. Mimi Nikiwa ni waziri wake itakuwa na sifa ya kiutendaji na bajeti yake. and board members wake ni manibu waziri wa kila wizara teule.
    Hii itasaidia uendeshaji na urahisishaji wa maamuzi ya Nchi. na kunsaidia Baba yetu JPOJM katika ufatiliziaji na utekelezaji ambao pia unakuwa katika meza ya Ofisi ya Waziri Mkuu. ( Hii ni pendekezo) Linahitaji kufikiriwa na Decisiom makers .
    Tanzania Kwanza na Uzalendo Mbele.
    Hapa Kazi Tu.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad