Chadema Longido Nayo Yasusia Kushiriki Kwenye Uchaguzi

Chadema Longido Nayo Yasusia Kushiriki Kwenye Uchaguzi
Kamati ya utendaji ya Chadema wilayani Longido imeunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa kutoshiriki uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 13 mwakani.

Uchaguzi huo utafanyika katika majimbo matatu ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini na baadhi ya kata nchini.

Kauli hiyo waliitoa siku chache tangu ushirika wa vyama vya Ukawa kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha uchaguzi huo ili kuruhusu wadau kukutana kujadiliana kilichotokea wakati wa uchaguzi wa udiwani Novemba 26.

Akizungumza na waandishi na habari jijini hapa jana, Mwenyekiti wa Chadema Longido, Alais Meing’arana alisema mazingira ya kisiasa kwa sasa hayaruhusu kufanyika uchaguzi huru na haki.

Pia, alisema Chadema inashangaa kuona Tume ya Uchaguzi kutangaza kurudiwa kwa uchaguzi jimbo la Longido wakati shauri lipo mahakamani kwa rejea ya kesi namba 35 ya mwaka 2017 katika Mahakama ya Rufaa.

“Hatutakuwa tayari kuona uvunjifu wa amani kwenye uchaguzi ujao kama tulivyoshuhudia uchaguzi wa marudio katika Kata 43 hasa jimbo la Arumeru Mashariki, watu walijeruhiwa wakiwa kwenye vituo vya kupigia kura huku mawakala wa Chadema wakizuiwa kusimamia kura za wagombea wao,” alisema Meing’arana.

Alisema hawana wasiwasi wa kurudiwa uchaguzi kwa sababu wana imani ya kushinda kwa kishindo iwapo tu, uchaguzi unaweza kufanyika katika mazingira yanayoakisi mshindi kutangazwa na si vinginevyo.

Katibu wa Chadema wilayani hapa, Mathayo Nyikin alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapaswa kushindana kwa hoja badala ya kutegemea kubebwa na vyombo vya dola.

Uchaguzi wa marudio wa ubunge Longido, umetangazwa baada ya NEC kutangaza jimbo hilo lipo wazi baada ya maelekezo ya Mahakama Kuu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad