Mtwara. Umewahi kujiuliza kwamba inaweza kuwapo zahanati inayotoa huduma kwa vijiji saba? Tena ikiwa na daktari mmoja?
Basi ipo zahanati moja katika kijiji cha Madimba wilayani Mtwara ambayo ina daktari mmoja huku ikitoa huduma kwa vijiji saba ikiwa ni pamoja na kuhudumia wajawazito.
Vijiji ambavyo vinapata huduma kwenye zahanati hiyo ni pamoja na Madimba, Namindondi, Mngoji, Mitembe, Mayaya, Mitambo na Mtendachi.
Zahanati hiyo ina daktari mmoja na watumishi wengine watatu akiwamo muuguzi mmoja, mkunga na mama afya.
Hata hivyo, wakati mwandishi wa habari hizi alipofika katika zahanati hiyo alimkuta mtumishi mmoja huku watatu hawakuwapo kutokana na kilichoelezwa kuwa ni majukumu mengine ya kikazi.
Akizungumza na Mwananchi, mjamzito Sharifa Khamis, mkazi wa kijiji cha Mtendachi alisema kuna wakati wanalazimika kushinda njaa kutwa nzima na hurudi nyumbani bila kuhudumiwa kutokana na wingi wa wagonjwa.
“Nimefika hapa tangu asubuhi, huduma ni kama mnavyoona mhudumu yuko mmoja anahudumia huko anarudi kule, akitoka kule anakwenda kule yaani hakuna huduma,” alisema.
“Siku nyingine tunakuja tarehe za kliniki zilishafika anaona watu ni wengi muuguzi anatuambia rudini mje kesho nishaelemewa na ukiangalia ni kweli inabidi tuondoke tu.”
Muuguzi wa zahanati hiyo, Veronica Haule alisema: “(Kwa) idadi tuko wanne, mganga, mkunga, mama afya na mimi muuguzi, lakini daktari sasa ana kitengo kingine cha kifua kikuu na ukoma kwa hiyo kituoni anapatikana mara mbili kwa wiki, mkunga yuko likizo anamaliza leo. Kwa hiyo kwa ndani ya mwezi mzima niko mwenyewe na mama afya hapa anapatikana kwa siku moja ,” alisema Haule.
Mkazi wa kijiji hicho, Athumani Ramadhani alisema zahanati kutokana na uchache wa watumishi wananchi wanalazimika kuwa wapole kwa kila jambo wanaloelezwa hata kama hawakubaliani nalo.
“Zahanati inahudumia vijiji saba na wahudumu hawatoshi mmoja anaweza kufanya kazi kutwa nzima, hata akigoma hatuwezi kumuonya kwa sababu anakuwa na uchovu,” alisema Ramadhani.
Akizungumzia kadhia wanayopata wagonjwa, mwenyekiti wa kijiji cha Madimba, Mohammed Mussa alisema zahanati hiyo inakabiliwa na uhaba wa watumishi kwa muda mrefu na walishachukua hatua lakini hakuna utekelezaji.
“Kama msimamizi wa masuala ya hapa kijijini nilionana na daktari wa hiyo zahanati akasema atafikisha hili suala kwa mganga mkuu wa wilaya zaidi ya hapo sijaona matokeo,” alisema.
Mratibu wa afya halmashauri ya Mtwara Vijijini, Elizabeth Mrope alisema zahanati hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi badala ya 13 aliodai kuwa wanahitajika wapo wanne.
Sera ya Afya ya 2007 inaelekeza kila kijiji kiwe na zahanati na kata kuwa na kituo cha afya vyenye watumishi wa kutosha. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Kata ya Madimba ilikuwa na wakazi 13,139 na kuna mradi mkubwa wa kuchakata gesi asilia unaoendeshwa na Kiwanda cha Madimba.
Source; Mwananchi