MFANYABIASHARA maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameanza rasmi kazi ya kuihudumia Klabu ya Simba.
Mo ameanza kuihudumia klabu hiyo baada ya kupita kwenye mchakato wa kumtafuta muwekezaji wa Klabu ya Simba kwa ofa yake ya shilingi bilioni 20 na kupata hisa kwa asilimia 50 huku 50 zikibaki kwa wanachama. Hata hivyo, bado kuna majadiliano na serikali ambayo inataka mwekezaji wa klabu asizidi asilimia 49.
Awali, mfanyabiashara huyo alikuwa anaihudumia timu hiyo kama mwanachama kabla ya kukabidhiwa na wanachama klabu hiyo na kuwa mwekezaji.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kutoka ndani ya timu hiyo, mfanyabiashara huyo ameanza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo mshahara, posho na mahitaji mengine.
Mtoa taarifa huyo alisema, kambi ya maandalizi ya mechi ya hatua ya pili ya Kombe la FA dhidi ya Green Warriors aliwezesha yeye kwa kuiweka timu ya Escape Two Hotel, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
“Ameanza kutoa huduma hiyo kwa kuanzia mechi dhidi ya FA kwa kufanikisha baadhi ya mahitaji muhimu ikiwemo kambi ya timu iliyoweka Escape Two Hotel.
“Pia anafanikisha baadhi ya mahitaji mengine ikiwemo mshahara na posho za wachezaji tukiwa katika matayarisho ya mechi hii ya FA tutakayocheza kesho (leo) dhidi ya Green Warriors,” alisema mtoa taarifa huyo.