Duka lingine la Nakumat lafungwa Baada ya Kutimuliwa Kwenye Jengo la Biashara.
0
December 08, 2017
Mzigo wa malimbikizo ya deni la pango leo Ijumaa ulisababisha wamiliki wa duka kubwa la Nakumatt Supermarket Tanzania la mjini Moshi, kutimuliwa kwenye jengo walilokuwa wakiendesha biashara.
Hili ni duka la mwisho kufungwa nchini baada ya maduka mawili kutoka jijini Dar es Salaam na Arusha kufungwa kutokana na wawekezaji hao kushindwa kumudu gharama za kuendeshaji.
Ilikuwa kama sinema asubuhi ya saa 3:00 baada ya kuonekana gari mbili za polisi zikiwa zimeimarisha ulinzi katika duka hilo lililopo barabara ya Kaunda, katikati ya eneo la kibiashara mjini Moshi.
Wateja waliotaka kuingia katika lango kuu kwa ajili ya kwenda kununua biadhaa, walijikuta wakizuiwa na walinzi wa kampuni binafsi ya Intelligence Security, wakiwa hawaelewi nini kimetokea.
Ilipofika saa 4:00 asubuhi, kulionekana harakati za wafanyabiashara waliokuwa wamekodishiwa maduka na Nakumatt Supermarket, wakiondoa bidhaa zao katika vyumba hivyo vya biashara.
Meneja Nakumatt Supermarket Tanzania, Alfrick Milimo alipoulizwa na Mwananchi amekiri kujulishwa kufungwa kwa duka hilo na kwamba ndio alikuwa anaelekea hapo kujua kulikoni.
“Mimi sikuwepo kwa hiyo sijui nini kinaendelea nimepigiwa tu simu kwamba tumezuiwa kufanya biashara. Ndio naelekea huko lakini kwa sasa siwezi kusema lolote maana sijui,” amesema Milimo.
Hata hivyo, Meneja wa Majengo wa Kampuni ya Erncon Holdings Ltd, Thadey Mariki inayomiliki jengo hilo amesema wamelazimika kumuondoa mwekezaji huyo kutokana na malimbikizo ya pango.
“Hatukuwa na namna nyingine bali kuchukua jengo letu. Nakumatt Supermarket wamekuwa wakiendesha biashara hapa lakini hawajatulipa kodi ya pango zaidi ya mwaka mmoja,” amesema.
Mariki amesema hatua hiyo ya Nakumatt Supermarket kutolipa kodi hiyo, kuliifanya kampuni yao iwe na hali ngumu ya uendeshaji ikiwamo kushindwa kulipa mkopo waliokopa kujengea jengo hilo
“Tulikopa benki ili kujenga jengo hili lakini tunashindwa kurejesha kwa wakati na kulipa kodi za Serikali kwa sababu ya malimbikizo hayo ya kodi ya Pango,” amesema bila kutaja kiwango wanachodai.
“Kabla hatujalifunga leo tuliongea na wafanyakazi wote wa Nakumatt na kuwaeleza hali halisi na kwanini tumechukua hatua hii. Tunatafuta mwekezaji atakayetoa huduma bora zaidi.”
Duka la Nakumatt Supermarket ambalo linamilikiwa na kampuni ya Kenya, ndilo lilikuwa duka kubwa na lililokuwa na wateja wengi kulinganisha na maduka mengine.
Mwananchi.
Tags