Emmanuel Okwi Amgomea Mzambia Simba

Emmanuel Okwi Amgomea Mzambia Simba
Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa, Emmanuel Okwi ndiye mchezaji pekee katika kikosi cha Simba hajatikiswa na ujio wa mchezaji wa kigeni Jonas Sakuhawa kutoka Zambia.

Lakini, mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ na Juma Luizio wanaweza kutikiswa na usajili wa Sakuwaha kutokana na nafasi zao wanazocheza.

Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zimeingia vitani kuwania saini za nyota wapya katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Novemba 15 na linatarajiwa kufungwa Desemba 15.

Miongoni wa klabu hizo ni Simba ambayo inataka kuongeza mchezaji mmoja wa kigeni ambaye ni Sakuhawa aliyetua nchini hivi karibuni kumalizana na vigogo wa miamba hiyo ya soka nchini.

Usajili wa Mzambia huyo umekuwa gumzo kwa kuwa klabu hiyo italazimika kumtema mchezaji mmoja wa kigeni ili apate fursa ya kusajiliwa katika dirisha dogo.

Lakini, usajili wa Sakuwaha unaonekana kutokumtisha Okwi, raia wa Uganda ambaye ana uhakika wa kuendelea kupata namba katika kikosi cha kwanza chini ya kocha Joseph Omog.

Mabao manane aliyofunga Okwi kwenye Ligi Kuu yanamuweka salama na hatakuwa na presha kubwa ya kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza Simba mbele ya Mzambia huyo ambaye rekodi yake kwenye soka ya Afrika ni moto wa kuotea mbali.

Sakuwaha aliyetua nchini wiki iliyopita kufanya majaribio ya kujiunga na Simba, anaonekana kulikosha benchi la ufundi la timu hiyo ambalo kwa sasa linasimamiwa na kocha msaidizi Masoud Djuma ambaye anashika kwa muda mikoba ya Omog ambaye yupo kwenye mapumziko.

Katika mazoezi ya Simba yanayoendelea katika kipindi hiki cha mapumziko ya ligi, Sakuhawa ameonyesha kiwango bora katika kufunga, kutengeneza nafasi za mabao, kumiliki mpira na kupiga chenga. Mzambia huyo anabebwa na umbo la miraba minne jambo linalompa nafasi kubwa ya kuziba nafasi ya mshambuliaji Laudit Mavugo anayehusishwa na mpango wa kutimkia Gor Mahia ya Kenya.

“Nimemtazama vizuri Sakuhawa baada ya kumsimamia katika majaribio ambayo ameendelea kufanya. Binafsi nimeridhika na kiwango chake kwa sababu ana sifa zote ambazo mimi kama kocha ninazihitaji kuziona kwa mshambuliaji wa kati ambazo ni kufunga na kutengeneza nafasi.

Kama ningekuwa mimi ndiye mwenye mamlaka ya mwisho kumsajili, ningekuwa nimeshafanya hivyo lakini viongozi wangu ndio wenye mamlaka hayo hivyo ni vyema kusubiri uamuzi wao,” alisema Djuma katika mazoezi ya jana asubuhi Coco Beach, Dar es Salaam.

Endapo Sakuhawa atamwaga wino, nafasi za kina Bocco, Liuzio, Mohammed Ibrahim ‘Mo’, Shiza Kichuya na Nicholas Gyan na wanapaswa kukaza buti kwani huenda Mzambia huyo akapangua kikosi cha Simba ili kuingia kwenye kikosi cha kwanza endapo ataendeleza makali.

Bocco na Luizio wanaocheza nafasi ya mshambuliaji wa kati wako kwenye hatari zaidi kwani wamekuwa wakipoteza idadi kubwa ya nafasi za mabao katika mechi mbalimbali ambazo Simba walicheza hivyo huenda wakajikuta wanarithi nafasi ya Mavugo benchi na kumpisha Mzambia huyo anayeonekana sio mchezaji wa kuanzia benchi.

Kichuya na Gyan wanaoshambulia kutokea pembeni wanaweza kuathirika pia na ujio wa mshambuliaji huyo hasa pale Simba itakapoamua kutumia mfumo wa 4-3-3 au 4-2-3-1 kwa kuwa Sakuhawa anaweza kusimama kama mshambuliaji wa kati na Okwi kusogezwa pembeni ambako ndipo anacheza mara kwa mara.

Ibrahim anaonekana hayuko kwenye presha kubwa analindwa na uwezo wa kucheza nafasi tatu tofauti uwanjani, lakini ile anayoipendelea ya kucheza nyuma ya mshambuliaji wa kati katika mfumo wa 4-4-2 inaweza kuathirika kwa kuwa Omog na benchi lake la ufundi wanaweza kumrudisha Okwi kwenye nafasi hiyo na Sakuhawa akacheza namba tisa.

Sakuhawa mwenye miaka 34 ambaye ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Zesco United ana uzoefu katika ligi tofauti za soka duniani.

Baada ya kutamba kwa miaka mitatu kwenye kikosi cha Zesco iliyomuibuka kuanzia 2006 hadi 2009, alicheza Ligi Kuu Ufaransa kwenye klabu ya Lorient aliyoichezea mechi 14 kuanzia 2009 hadi 2010 kabla ya kujiunga na Le Havre ambapo hakufanya vizuri akicheza mechi nne tu.

Mwaka 2011 alijiunga na El Merreikh ya Sudan aliyocheza mechi 33 na kufunga mabao 22, alidumu miaka miwili kabla ya kutua TP Mazembe Englebert aliyoifungia mabao 14 na baadaye mwaka 2014 alirejea Zesco United.

Akizungumzia usajili wa Sakuhawa, meneja wa Simba, Robert Richard alisema unasubiri ripoti ya kocha Omog.

“Kuna mahitaji ambayo kocha ameupatia uongozi ambayo ndio yatakayofanyiwa kazi, hivyo ndani ya kipindi hiki, kamati ya usajili itakutana kufanyia kazi ripoti.

Kama kapendekezwa atasajiliwa kama hajapendekezwa hatasajiliwa,” alisema Richard.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad