Gari la Maafisa Misitu Latekwa

Wachimbaji haramu wa madini zaidi ya 100 waliokuwa wakifanya shughuli hiyo kinyume cha sheria katika hifadhi ya msitu wa Mazingira asili wa Amani uliopo wilayani Muheza wameliteka gari aina ya Land Cruser la maafisa misitu wa hifadhi hiyo kisha kutaka kulichoma moto katika jaribio lao la kupambana na wahifadhi waliokuwa doria ili kuzuia uchimbaji haramu wa madini katika hifadhi hiyo.

Wakizungumza katika hifadhi hiyo afisa misitu katika hifadhi ya Amani Justine Sayi amesema mara baada ya kuliteka kisha kuwafukuza bila mafanikio watendaji wa wakala wa huduma za misitu wa hifadhi hiyo ambao walikimbilia porini hadi eneo la Ubiri lililopo wilayani Korogwe walipata taarifa ndipo walipoomba msaada wa Jeshi la Polisi na kulikuta gari limetelekezwa huku matairi mawili yakiwa yametolewa upepo baada ya wasamaria wema kuwasihi wachimbaji hao wasilichome moto na wala kulisukuma katika bonde kubwa lilipo pembeni mwa barabara.

Hata hivyo akizungumza na viongozi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi ya msitu wa mazingira asili Amani,Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Muheza Eng' Mwanasha Tumbo amesema tayari watu 13 wametiwa mbaroni na jeshi la polisi na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kwa watuhumiwa.

Kufuatia hatua hiyo,Mhifadhi mkuu wa hifadhi ya msitu wa mazingira asili Amani Mwanaidi Kijazi amesema ili kuchochea hamasa ya ulinzi katika hifadhi hiyo wametoa gawio la asilimia 20% ya mapato yatokanayo na utalii kwa viongozi wa serikali za vijiji,wakuu wa shule zinazozunguka hifadhi hiyo kisha kuwanunulia vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kuimarisha miundo ya shule na zahanati katika maeneo yao pamoja na vifaa vya mionzi ya jua kwa ajili ya kuwasha taa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad