Hivi Ndivyo Tukio la Kukamatwa Dola Milioni 1 Uwanja wa Ndege Lilivyokuwa

Hivi Ndivyo Tukio la Kukamatwa Dola Milioni 1 Uwanja wa Ndege  Lilivyokuwa
Polisi Kitengo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), inawashikilia watu wawili akiwamo raia wa Uganda kwa tuhuma za kukutwa na dola 1 milioni za Marekani.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Matanga Mbushi alisema jana kwamba fedha hizo zilikuwa zikitokea Uganda na ziliingizwa nchini kinyume cha taratibu.

Aliwataka watuhumiwa hao kuwa ni Wilfred Usangi, raia wa Uganda na mlinzi wa kampuni ya kusafirisha fedha ya SGA, Meshaki Sangwa.

Kamanda Mbushi alisema hayo jana baada ya kuulizwa na mwandishi wetu kauli iliyotolewa awali na Rais John Magufuli kuhusu fedha hizo alipokuwa akifungua tawi la Benki ya CRDB mjini Dodoma.

“Pia nataka mdhibiti matumizi ya dola, hivi ninavyozungumza kuna dola milioni moja zimekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, hakuna maelezo yoyote juu ya kuingia fedha hizo, ni lazima tuwe makini,” alisema Rais Magufuli.

Kamanda Mbushi alisema watuhumiwa walikamatwa Desemba 11, saa 2:30 usiku wakiwa eneo la ukaguzi uwanjani hapo.

Alisema raia huyo wa kigeni aliwasili nchini kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya akitokea Uganda akiwa na fedha hizo ambazo alikuwa akizipeleka katika Benki ya Stanbic bila kuthibitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). “Hawa wamekuwa na mazoea ya kusafirisha fedha mara kwa mara bila ya kufuata utaratibu. Alitakiwa achukue fomu, ajaze fedha walizokuwa nazo ili maofisa wa TRA wathibitishe lakini hawakufanya hivyo,” alisema.

Kamanda Mbushi alisema watuhumiwa bado wanashikiliwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad