Mbunge wa Nzega Mjini Mh. Hussein Bashe amemtaka kocha mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM na Makocha wasaidizi kuwa na umoja na ushirikiano ili kufikia malengo ya Chama na Serikali.
Bashe ametumia ukurasa wake wa ‘Twitter’ kuwasilisha ombi lake hilo kwa uongozi wa juu ambao ulichaguliwa jana kwenye mkutano mkuu wa tisa wa Chama mjini Dodoma ambapo Mwenyekiti Rais Magufuli amechaguliwa kuongoza kwa miaka mitano.
“Kocha na Makocha wasaidizi Tunaamini Tumewaamini Tuliwaamini Kila la kheri ktk kukiongoza Chama Chetu 2017-22. (Alone we can do so LITTLE, together we can do so MUCH" Team work We rise by lifting others appreciating others and respecting others)”, ameandika Bashe.
Katika maneno yake ya Kiingereza Bashe amehimiza kufanya mambo kwa umoja ili kupiga hatua kubwa tofauti na mtu akifanya vitu peke yake atapiga hatua kidogo. Uongozi huo mpya utahudumu kwa miaka mitano 2017 hadi 2022.
Rais Magufuli alichaguliwa kwa kura zote 1821 za wajumbe wa mkutano mkuu. Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar pia alichguliwa katika nafasi ya Mwenyekiti Zanzibar wakati nafasi ya Makamu Mwenyekiti alichaguliwa Ndugu Philip Mangula.