Msanii mkongwe wa filamu bongo ambaye ni maarufu kwa kuibua vipaji vya wasanii wengine, Jacob Steven au JB, amesema wao kama wakongwe wa sanaa walifanya makosa kumtengeneza Gabo peke yake.
Akizungumza kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, JB amesema kitendo cha kumtengeneza Gabo peke yake kwa kipindi ambacho alianza kuwa kwenye 'pick', walitakiwa kuwatengeneza kina Gabo wengine kama watatu, ili kuweza kuleta changamoto zaidi kwenye tasnia ya filamu.
JB ameendelea kwa kusema kwamba hata ukiangalia historia ya sanaa ya bongo movie, walianza na 'intake' ya marehemu Kanumba na Ray, kisha wakaja kizazi cha kina Hemedi Suleiman na Yusuph Mlela, lakini kipindi cha Gabo hakukuwa na wengine ambao wangeweza kusimama kwenye soko na kuleta ushindani wa kazi, hivyo kumfanya Gabo asimame peke yake licha ya uwezo mkubwa alionao kwenye sanaa.
“Unajua tulifanya makosa kwa Gabo, tulifanya makosa makubwa sana, kipindi ambacho tulimtengeneza Gabo tulitakiwa kuwatengeneza kina Gabo wengine kama watatu hivi, nasema hivi kwa sababu ukiangalia kwenye bongo movie kuna intake ambazo zilikuwa zinaleta ushindani mkubwa sana kwenye soko, kulikuwa na kizazi cha Kanumba na Ray, kikaja kizazi cha kina Hemedi Suleiman na Yusuph Mlela, lakini kwa Gabo amekuwa peke yake, sisesemi kwamba hakuna wengine, ila ukiangalia ile trend tulipaswa kufanya hivyo ili kuleta changamoto na ushindani kwao, matokeo yake Gabo ndiye anaonekana bora kuliko wengine”, amesema Jacob Steven.
Licha ya hayo JB amekiri kuwa Gabo ndiye muigizaji bora kwa sasa, na ndiye ambaye yupo kwenye 'pick' kama ambavyo alikuwa marehemu Kanumba.