Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeandaa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwa maofisa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mazoezi hayo yaliyopewa jina ‘Ushirikiano imara’ yanawashirikisha wanajeshi na maofisa wa Serikali kutoka Tanzania, Uganda, Burundi, Kenya na Rwanda.
Mkuu wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi, Brigedia Jenerali Alfred Kapinga amesema leo Jumanne Desemba 5,2017 kuwa watu 300 wanashiriki wakiwamo makamanda wa jeshi na maofisa wa juu kutoka wizara zaidi ya tatu ikiwamo ya Katiba na Sheria.
Amesema kwa Tanzania wanaoshiriki ni makamanda na maofisa watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Brigedia Jenerali Kapinga amesema kwa upande wa Tanzania washiriki ni 107 na kwamba, mazoezi yameanza jana Desemba 4,2017 na yatazinduliwa Desemba 7,2017 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
“Mazoezi yanafanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Kunduchi, Dar es Salaam na yamejikita katika mambo makuu manne,” amesema.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni operesheni katika ulinzi wa amani; kupamba na ugaidi; kupambana na uharamia wa aina yoyote ndani ya Bahari ya Hindi; na majanga na maafa.
Amesema lengo la mazoezi hayo ni kuwaandaa na kuwapa uwezo washiriki katika kupanga na kutekeleza majukumu ya operesheni za ulinzi wa amani katika kupambana na ugaidi, uharamia na kukabiliana na maafa.