Vikumbo vya kuwania ubunge katika majimbo ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini vimeanza kwa idadi kubwa ya makada wa CCM kujitokeza kuchukua fomu.
Katika jimbo la Singida Kaskazini ambalo liko wazi baada ya Lazaro Nyalandu kujiuzulu na kujivua uanachama wa CCM kisha kuomba kujiunga na Chadema Oktoba 30 kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo ndani ya chama hicho tawala, tayari wagombea 17 wameshachukua fomu akiwamo aliyekuwa msaidizi wake.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) majimbo hayo yatafanya uchaguzi Januari 12 mwakanina mchakato wa kupata wagombea ndani ya CCM ulianza Desemba 5 na unatarajiwa kukamilika kesho.
Katibu wa CCM Wilaya ya Singida Vijijini, Grace Shindika alisema jana kuwa miongoni mwa wanachama waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Elia Digha ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo.
“Watu wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi hii kuliko ilivyokuwa katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2015. Karibu wote wamechukua na kujaza kisha kurejesha isipokuwa wanachama wawili tu ndio hawajarejesha fomu zao,” alisema.
Alisema hakuwa katika nafasi ya kutaja majina ya watu wote walioomba kukiwakilisha chama na kwamba miongoni mwao pia ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya wa Singida Vijijini, Narumba Hanje.
Mwingine aliyejitosa kutaka kupewa ridhaa ya CCM kuwania jimbo hilo ni Haidel Gulamali ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Uchumi wa chama hicho Mkoa wa Dodoma. Pia, Gulamali aliwahi kuwania kuteuliwa na chama hicho kugombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini mara mbili bila mafanikio.
Kwa mara ya kwanza, Gulamali aliingia katika mchakato wa ndani ya CCM kuwania ubunge wa Dodoma Mjini kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambako alishika nafasi ya saba kati ya wagombea kumi na moja na katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambako alishika nafasi ya pili.
Songea na Longindo
Katika jimbo la Songea Mjini, tayari wanachama wanne wa CCM wameshachukua fomu za kugombea ubunge kuziba pengo lililotokana na kifo cha Leonidas Gama aliyefariki dunia Novemba 23.
Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu wa CCM wilaya ya kichama ya Songea Mjini, Juma Mpeli alisema wanachama hao wamechukua fomu tangu juzi na jana mchana huku akibashiri kwamba wanachama wengi zaidi watajitokeza kuwania nafasi hiyo.
Waliochukua fomu ni John Nchimbi, Gideon Ole Lairumbe ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Veta, Mussa Ndomba pamoja na Kayoya Fuko.
Pamoja na kutangazwa kwa tarehe ya uchaguzi katika Jimbo la Longido, kujaza nafasi ya aliyekuwa mbunge wake kupitia Chadema, Onesmo ole Nangole, hadi jana hakuna mwanaCCM aliyekuwa amejitokeza kuwania nafasi hiyo. Ole Nangole alivuliwa ubunge baada ya Mahakama Kuu kutengua ushindi wake kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2015.