Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo amewataka wakristo wote na watanzania kwa ujumla kudumisha amani kwa sababu ni tunu inayoliliwa na mataifa yote ulimwenguni.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo
Amesema amani haiwezi kuja bure bali kila mtanzania anatakiwa kufanya kazi inayompendeza Mungu usiku na mchana ndipo amani itapatikana. “Kila mtanzania anatakiwa kufanya kazi inayoleta utukufu kwa Mungu kwani ndiyo kazi pekee inayoweza amani na utulivu,” amaesema Pengo.
Askofu Pengo ameyasema hayo katika Mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Maurus Kurasini jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za Mkesha wa Krismas ambapo alizaliwa Mwokozi Yesu Kristo.
Amesema hakuna njia ya makato ya kuleta na kudumisha amani Tanzania na duniani kwa ujumla zaidi ya kufanya mambo yenye kumpendeza na kumtukuza Mungu. Amemshukuru Rais John Magufuli kwa kuifanya nchi kuwa na amani na mshikamano na amewataka watanzania kila mtu na imani yake kumwombea Rais ili aendelee kuiongoza nchi katika maendeleo anayohitaji Mungu.
Aidha Askofu Pengo amesema kuwa anatambua juhudi zinazofanywa na mataifa mbalimbali na watu mashuhuri kuleta amani duniani lakini akawakumbusha watanzania kuwa ni bora amani inayojengwa na watanzania wenyewe kuliko amani ya kuletewa.
Kwa upande wake Father John Sembuyagi wa Kanisa la Anglikana Tanzania ambaye alikuwa Mgeni Mwalikwa kutoka Jimbo Kuu Dodoma, Dawati la Theolojia amewataka wakristo Tanzania kujenga mazoea ya kuwapeleka watotowao kanisani ili kuwaweka karibu na Mungu. Sembuyagi ameyasema hayo wakati akitoa salamu za mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam.
Amesaema njia pekee ya kuwafanya watoto wetu waseme na Mungu ni kupitia mafundisho kanisani hali inayowasaidia kumjua Mungu na yale yote yanayompendeza na yale yote aliyokataza.
“Tusimfanye Mungu akae kimya juu ya watoto wetu, tusimfanye Mungu akae kimya juu ya familia zetu, tusimfanye Mungu akae kimya juu ya nchi yetu tumfanye Mungu aseme na watoto wetu na familia zetu ili tuwe na viongozi mahiri wa kanisa hapo baadaye,” amesema Sembuyagi.
Kadinali Pengo Amewataka Wakristo na Watanzania kwa Ujumla Kudumisha Amani
0
December 25, 2017
Tags