SIKU chache baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari wa Tiba za Michezo Tanzania (Tasma), Nasoro Matuyza kutangaza kuomba wadau wamchangie kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko raia wa Zimbabwe, kumezua mtafaruku wa aina yake.
Matuzya ambaye amewahi kuwa daktari wa Yanga mara kadhaa alitoa taarifa ya maombi hayo mtandaoni na kueleza kuwa Kamusoko ana tatizo kubwa la goti lakini anaweza kumsaidia endapo kiwango fulani cha fedha kitapatikana.
Alisema kufanikisha matibabu ya Kamusoko, inahitajika Sh 720,000 ili kutibu tatizo la kupasuka kwa kikombe cha ndani cha mguu wa kushoto akitolea mchanganuoa wa fedha hiyo alisema Sh 480,000 kwa kipimo cha MRI, Sh 158, 000 dawa na vifaa tiba na Sh 82,000 ya X Ray, Ultra Sonic Sound pamoja na kumuona daktari.
Akizungumza juu ya kilichotokea baadaye alisema: “Nimeamua kuachana na Kamusoko hadi hapo baadaye uongozi utakaponikabidhi, nilitoa taarifa ile kwa nia njema lakini kuna watu wamenishambulia na kuniona natafuta fedha kinguvu.”
Alipotafutwa Daktari wa Yanga, Edward Bavo alisema: “Hizo taarifa za mitandaoni mimi sizipendi, Kamusoko yuko fiti na alikuwa aanze mazoezi lakini kwa kuwa ligi imesimama, ataanza pamoja na wenzake, sijaonana naye kwa siku kadhaa, sijui chochote kuhusu taarifa za Matuzya unazoniambia.”
Walipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa na Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten hawakupatikana.