Viongozi wastaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jana waliutumia Mkutano Mkuu wa chama hicho kueleza kilipo na kinapoelekea, huku Rais mstaafu Jakaya Kikwete akisema hakuna shule ya urais na uenyekiti.
Kikwete ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa CCM akiwa wa kwanza kutoa salamu aliueleza mkutano huo mjini Dodoma kuwa nafasi hiyo hakuna anayesomea ila mhusika anasoma akiwa ndani.
Alisema alitambua fika kuwa Rais John Magufuli ndiye mtu anayestahili kwenye nafasi hiyo licha ya kupata maswali kutoka kwa watu walioonyesha wasiwasi. “Nilimtetea Magufuli watu walihoji hajawahi kuwa hata mjumbe wa shina iweje ghafla aje kuwa mwenyekiti wa chama. Nikawaambia ataweza kwani hahitaji shule,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili, Rais Magufuli amefanya mambo makubwa yanayoleta matumaini na ameonyesha ujasiri wa hali ya juu.
“Mpaka sasa ‘big up’ mtani wangu. Kazi hii ngumu sana, sababu mimi nimeifanya. Katika kazi ngumu duniani hii ndiyo kiboko. Uzuri na ubaya wa kazi hii ina upweke mkubwa,” alisema.
Kuhusu malalamiko ya hali ngumu ya maisha Kikwete alisema, “Kuweni na subira, viongozi wetu makini wanatambua matatizo yanayowakabili wananchi na ninaamini wanayatafutia ufumbuzi.”
Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM aligusia mwenendo wa chama hicho na kueleza kuwa wastaafu wanafarijika hali ya chama ikiwa shwari.
“Sisi tuliostaafu faraja yetu kubwa ni kuona chama chetu kinaendelea kuwa imara. Tukija kwenye mikutano na watu wanafurahi na sisi mioyo inakuwa baridi. Lakini tukisikia mivurugano kwenye chama tunaweza pata magonjwa ya moyo,” alisema.
Kauli ya Kikwete haikupishana na aliyoitoa waziri mkuu mstaafu, Mizengo Pinda aliyesisitiza usimamizi wa nidhamu ndani ya chama na Serikali.
Pinda alimtaka Magufuli kutosita kuchukua hatua ndani ya chama na Serikali endapo ataona wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
“Nimefurahishwa na namna ulivyosimamia kupambana na rushwa. Nina imani umepata viongozi wasafi ambao hawatakuwa wakisemwasemwa. Ukimpata ambaye haeleweki si mbaya unamtoa na kumuweka mwingine,” alisema.
Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Yusuph Makamba aliamsha shamrashamra alipopanda jukwaani na kummwagia sifa Magufuli. “Tunakufahamu kuwa wewe una uwezo mkubwa kwa kazi ya urais na ndiyo maana Kamati Kuu ilipokutana ikakupendekeza. Wewe ndiye unastahili kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kuwa moja ya matatizo tunayoyapata ndani ya CCM ni watu kutosema ukweli, wanageuza matatizo, fitina ndiyo ukweli,” alisema.
“Kuna siku nilikutumia meseji ukaniambia ushauri mbovu huutaki, hivyo ndivyo inavyotakiwa, mimi sikukasirika.”
Makamu mwenyekiti wa CCM Bara mstaafu, Samwel Malecela alisema, “Wenzetu wanaongoja kama fisi mkono udondoke watachukua muda mrefu sana maana chama chetu kipo vizuri.”
Alipotoa salamu, makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Amani Abeid Karume alipongeza watu wapya waliochaguliwa kuingia kwenye uongozi wa chama hicho.
Kikwete Afunguka Alivyompigania Magufuli Kuwa Mwenyekiti
0
December 19, 2017
Tags