Kuelekea 2018:Barua Yangu Kwa Rais Wangu Dr John Pombe Magufuli

Mheshimiwa Rais,

Pongezi kwa kumaliza miaka miwili na zaidi madarakani na pongezi za dhati kwa vita dhidi ya rushwa ambayo umepigina nayo toka siku ulipoapishwa na kuonyesha mwelekeo mwema.

Mheshimiwa Rais, tukiwa tunaelekea kufunga mwaka 2018, mimi kama mwananchi na mpiga kura ningependa kuona serikali ikiwaangalia kwa jicho la karibu matajiri wa Tanzania wanaomiliki biashara mbalimbali ambao utajiri wao wameuficha nje ya nchi.

Mheshimiwa Rais, ni lazima kila Mtanzania afahamu, hata kama wengine watafahamu kwa shingo upande kwamba tunaimini nchi yetu na taasisi zake kiasi kwamba tunaweza kuwekeza maisha yetu, mali na fedha zetu hapa nyumbani. Hii ndio njia pekee ya kuipelekea nchi mbele pamoja na jitihada za kupambana na rushwa ambazo zinatekelezwa.

Mheshimiwa Rais, hali ilivyo sasa bado ni tofauti. Wapo baadhi ya raia ambao hawaijali nchi wala hawajali kuhusu mafanikio yake. Raia hawa wanatengeneza mabilioni ya fedha wakiwa Tanzania lakini baada ya hapo wanakwenda kuwekeza katika vitu vikubwa nje ya nchi. Tanzania haipati faida yoyote na hii ni moja ya mambo ambayo yamechangia kudorora kwa kiwango cha maisha ya Mtanzania wa kawaida.

Mheshimiwa Rais, najua unafahamu kuwa wafanyabiashara wengi wakubwa walitajwa katika sakata la Panama wakiwa ni miongoni mwa watu wenye akaunti katika taasisi za kifedha za nje ya nchi ili kuficha utajiri wao, utajiri ambao umepatikana hapa nchini, kwa rasimali zetu, miundombinu yetu, nguvu kazi yetu, na wakati mwingine hata mitaji toka taasisi zetu za fedha au taasisi za nje za fedha kupitia jina la nchi yetu.

Mheshimiwa Rais, ni vigumu sana kuwaamini hawa watu. Wanapambana kwa mbinu yoyote ili kujikusanyia mali kutoka kwa watanzania wanyonge wanaofanyakazi kwa bidii na kutoa faida kidogo sana wanayopata kurejesha kwa jamii.

Mheshimiwa Rais, nakumbuka kupitia gazeti la The Citizen lilivyoripoti jinsi Watanzania wengi walivyokamatwa katika sakata la Panama Papers mwaka 2016. Nimekuwa nikiwaza ni kiasi gani taifa limekuwa likipoteza. Sakata la kuvuja nyaraka la hivi karibuni la Paradise Paper limeibua tena hasira zangu juu ya suala hili.

Mheshimiwa Rais, juma lililopita niliona taarifa iliyoandikwa kwa kina namna Yusuf Manji (mmoja wa Watanzania 45 wanaotumia akaunti za nje kuficha utajiri wao) alivyojikusanyia fedha kutoka TANESCO ndani ya mwaka mmoja kupitia zabuni, zaidi ya shilingi bilioni 100.

Mheshimiwa Rais, najiuliza kuna mtu yeyote amefanya uchunguzi kujua kama hizi fedha zilitumika kwa njia sahihi? Au huduma aliyoitoa kama sehemu ya zabuni ilikidhi vigezo vilivyotakiwa? Kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, hata ndugu zake pia walitajwa katika sakata la Panama.

Mheshimiwa Rais, wala huhitaji intelijensia kubwa kujua baadhi ya mambo, mfano ukipekua kupitia Google utaona ana mali mbalimbali nchini Marekani. Hili, ukiongeza na kwamba alitajwa katika sakata la Panama, linanifanya mimi kuwa na mashaka na malengo ya biashara yake yoyte nchini Tanzania. Huyu ni mtu mmoja tu, wako mamia hapa nchini.

Mheshimiwa Rais, TAKUKURU na TRA wanajukumu la kuhakikisha kama fedha za umma walizopewa watu hawa kufanya kazi za umma zilitumika katika namna inayokubalika, kuanzia huduma iliyokusudiwa, kodi, namna zabuni ilivyopatikana, faida ilivyotumika na kadhalika.



Mheshimiwa Rais, 2018 pia nakuombea uwe mwaka ambao utaacha kuteua watu ambao lazima uwe unarudi tena kuwakumbusha kufanya kazi zao. Najiuliza mara nyingi kwamba umeteua mtu, umempa majukumu lakini bado inabidi urudi tena kumkumbusha cha kufanya na bado yuko pale pale. Mfano hili jambo la video zisizo na maadili, Waziri hatazami TV hadi urudi tena umkumbushe? Mbona ana wasaidizi lukuki na kodi zetu tunawalipa? Mbona anakuchosha na una mengi ya kufanya? Ishu ya Bandari na zile flow meters? Kweli hadi Rais urudi tena bandarini kukagua personally? Hii si fair kwako Mheshimiwa na kwa nchi. If people can’t deliver they need to quit. Tunahitaji muda wako utusaidie mambo mengi. Hawa watu wanakuchosha kwa kila wakati kuwakumbusha ya kufanya.

Mheshimiwa Rais, ningependa kuandika zaidi lakini naomba nikuache na hili kwanza. Nitaandika tena wakati mwingine.



Wako katika ujenzi wa Taifa

Uhuru Wanzagi,

Musoma, Mara, Tanzania
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kwa kweli maoni safi kabisa na tamani muheshimiwa raisi mchapa kazi namba wa taifa hili huu ujumbe umfike. Kwa kuongezea tu ni kwamba nchi yetu tayari imeshatumia trillion of money ambazo ziko site katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kuhakikisha maisha ya mtanzania yanaboreka kwa hivyo tungeomba taasisi au wizara husika kukadhania kutoa elimu husika kuwajuvya wananchi kiundani na kiufasaha jinsi serikali yao ilivyokwishaekeza kiasi kikubwa cha utajiri wa pesa zao zinazopatikana kwa ajili ya kuleta faida kubwa zaidi itakayowafaidisha watanzania wote. Watanzania lazima waelimishwe juu ya jitihada za serikali katika kupambana na vita ya umasikini. Na kama watanzania hawataelimishwa na kuhamasishwa vya kutosha juu ya jitihada hizo za dhat za kimaendeleo basi wataelimulishwa na wasaliti ambako kutakuwa ni kupotoshwa na wasiliti na kwa hafla tu ukiangalia wakati mwengine utaona yakuwa kana kwamba wasaliti wana mikakati iliojipanga zaidi kufikisha ujumbe wao potofu kuliko ukweli halisi. Shetani si lazima ajitokeze kwa sura ya kutisha ili ujuwe kuwa ni shetani hapana kwani anaweza kuja kwa sura jamili kabisa na madhara yake yakawa maafa makubwa. Nimetoa mfano huu wa shetani ili kutoa tahadhari ya baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati wa kuwatetea mambo kadhaa wa kadhaa katika kumkosoa muheshimiwa raisi katika juhudi zake za kulipigania Taifa kimaslahi kwa wote. La kushangaza zaidi mtu huwezi kuendesha harakati nzito za kuyafunika mazuri mengi yaliyofanywa na muheshimiwa raisi ili yaonekane si chote chote si lolote na badala yake uyatangaze mabaya yake machache alafu mtu huyo atoke kifua mbele na kujitangaza kuwa yeye ni wanaharakati wa kulitetea taifa hili huo ni unafiki uliopindukia ni usaliti na ni shetani aliejileta kwa sura ya mtu kueneza maovu ili watu waache kuunga mkono mambo ya manufaa juua ya maisha yao na vizazi vyao. Mtanzania na watanzania ili kushinda vita y kujikomboa na umasikini wakati ndio huu lazima tumuunge mkono kiongozi wetu wa nchi. Maghufili ni mtu safi sana ni mpiganaji aliejitoa kwa kwa nchi yetu . Watanzania tulimshinda Iddi Amin si kwa sababu tulikuwa na nguvu hapana ni umoja na uzalendo wa watanzania wakati ule ulikuwa sio wa kimchezo mchezo. Radio zilipiga nyimbo za hamasa masaa ishirini 24 bila kuchoka. Kwaya mashuleni kote nchini zilihubiri utaifa na hasira juu ya nduli Iddi Amin na watanzania waliapa lazima Amini atashika adabu na kweli Amini alishika adabu na kwa muda mfupi historia iliyokosa kuandikwa lakini Uganda ikawa moja ya sehemu ya Tanzania na Tanzania ingekuwa nchi ya kizungu pengine mpaka sasa Uganda ipo chini ya utawala wa tanzania. Sasa tujiulize nani katuroga hata tunashindwa kuungana na kuhamasishana kumuunga mkono muheshimiwa raisi na serikali yake au tuseme kuiunga mkono nchi yetu kupambana na adui hatari zaidi adui umasikini? Heri za mwaka mpya.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad