Ikiwa ni takriban siku sita tangu mlimbwende maarufu Bongo, Wema Sepetu ang’atuke Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Jonathan Lema ameibuka na kuzungumza mambo yaliyokuwa nyuma ya pazia kumhusu mrembo huyo.
Wema alitangaza uamuzi wake wa kukihama Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), Ijumaa iliyopita kupitia ukurasa wake wa Instagram.
CHANZO CHAVUJISHA
Awali, chanzo makini kilicho ndani ya Chadema, kilieleza kuwa, miezi michache baada ya Wema kujiunga na chama hicho, ilibainika ni mchanga sana kisiasa tofauti na walivyotarajia.
KUMBE WALIJUA WEMA ‘MWANAFUNZI’
Kilisema baada ya kubainika hivyo, Chadema walijua kabisa kuwa anaweza kubadilika wakati wowote hivyo waliona anahitaji kupewa darasa la kisiasa ili aweze kuwa imara. Chanzo hicho kilienda mbele zaidi kwa kusema, ililazimika baadhi ya viongozi wazoefu wa chama hicho kuchukua jukumu la kumkuza kisiasa.
Wema Sepetu.
ALIANZA KUKUZWA KISIASA
“Viongozi mbalimbali tu wakaanza kumpa darasa. Waligundua alipokuwa CCM hakuwa anaijua siasa wala kuwa na ule ujasiri wa kuwa mpinzani, wakaanza kumjenga,” kilidai chanzo hicho.
Kilipobanwa zaidi chanzo hicho ili kiweze kuwaweka bayana viongozi hao ambao walijitolea kumfundisha mrembo huyo ndipo aliposema ni viongozi tofauti, akiwemo mbunge wa Arusha, Lema.
“Ni viongozi wengi tu ambao wengi wao walikuwa ni wa ngazi ya chini lakini kwa ngazi za juu, Mbunge wa Arusha Mjini (Lema) kipindi kile alipokwenda kumtambulisha kwa mara ya kwanza jimboni kwake,” kilizidi kudai chanzo hicho.
HUYU HAPA LEMA
Amani lilimtafuta Lema kupitia simu yake ya mkononi ambapo awali, aliomba asimzungumzie mrembo huyo kwani hana umuhimu wowote mkubwa ndani ya chama.
Mwanahabari wetu alipozidi kumuomba tena na tena amzungumzie japo kwa yale ambayo tayari chanzo makini kilikuwa kimeshalieleza Amani, Lema akafunguka ambayo watu hawajui kuhusu Wema:
“Huyo (Wema) hakuna sababu ya kumzungumzia sana. Kwanza kama watu wanafikiri alikuja akiwa anaijua siasa na pengine ni faida kwetu waelewe si kweli. Alikuwa mtupu sana. Kwa hiyo kuchukua muda wangu kumuongelea ni kumpa popularity (umaarufu) asiostahili kabisa na ninyi wanahabari mtusaidie kuepuka haya mambo.”
ATHIBITISHA KUFUNDISHWA
“Alikuja kufundishwa siasa. Hakuwa akijua chochote. Mimi nafikiri tusipoteze muda sana kumjadili maana hata katika mafunzo tulijua kwamba anaweza kubadilika na kweli amebadilika,” alisema Lema.
AANIKA JINSI MKEWE ALIVYOMNOA
Akizidi kushusha dondoo za mrembo huyo, Lema aliweka bayana kuwa kuna mambo mengi ambayo watu hawayajui kuhusu namna mrembo huyo alivyokuwa anafundwa na mkewe.
“Naweza kukutumia video fupi (clip) ya mke wangu Neema uone namna ambavyo alikuwa akimfundisha na kumuongoza kwa mambo mengi ya kisiasa na maisha kwa ujumla (hakutuma video yenyewe), muhimu ndugu yangu (akilitaja jina la mwandishi wetu) tusaidiane kukuza demokrasia na siyo kupoteza muda kwa mambo yasiyokuwa na tija kama hayo.
“Katika maisha kuna watumwa wa aina tatu, kuna watumwa wanakula keki, kuna watumwa wanakula mkate na kuna watumwa wanakula mihogo mibichi, wote hao ni watumwa,” alisema Lema bila kufafanua maana ya mfano huo na kuongeza;
“Sema wakati tunategemea anaweza kuelekea kuzuri na akiwa hajaiva vilivyo, huyooo akahama. Tumuache tu bwana hakuna hata sababu ya kutumia nguvu nyingi kumzungumzia mtu ambaye ndio kwanza ni mwanafunzi na hana uzito wa kushtua kama ambavyo watu wanataka kutengeneza,” alisema Lema.
MBOWE VIPI?
Amani lilimtafuta Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Aikaeli Mbowe ili kumsikia anamzungumziaje mrembo huyo ambaye wengi waliamini alikuwa na mchango katika chama hicho, lakini alipopatikana alimpuuza na kuomba aulizwe mambo ya msingi ya kitaifa.
“Huyo mimi siwezi kumzungumzia. Kama una jambo la kitaifa unaweza kuniulizia lakini kwa huyo achana naye,” alisema Mbowe.
TUMEFIKAJE HAPA
Februari mwaka huu, Wema na mama yake ambao walikuwa wafuasi waaminifu wa CCM, walitangaza kung’atuka katika chama hicho na kujiunga na Chadema kwa kile walichodai kwenda kuifanya demokrasia ya kweli.
Uamuzi huo waliufanya ikiwa ni siku chache baada ya mrembo huyo aliyeipigia CCM kampeni katika uchaguzi wa mwaka 2015 atajwe kwenye orodha ya wasanii wanaojihusisha na masuala ya madawa ya kulevya.
Kupitia sakata hilo, Wema hadi sasa anakabiliwa na kesi ya madawa ya kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.