Mbunge wa jimbo la Kilombero kupitia Peter Lijualikali ameachiwa kwa dhamana baada ya kukamatwa na maofisa wa polisi akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro.
Kabla ya kuachiwa kwa dhamana Lijualikali ambaye anakabiliwa na kesi iliyoko mahakamani ya ushawishi na kuchoma moto ofisi ya serikali ya kijiji cha Sofi Malinyi amehojiwa kwa saa kadhaa katika kituo cha polisi mkoani Morogoro.
Akieleza leo Desemba 22 sababu za kukamatwa kwa mbunge huyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Matei amesema anatuhumiwa kwa kosa la kimtandao ambalo ni kusambaza picha za mtu anayedai kuwa anataka kumuua jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kamanda Matei amesema kuwa baada ya kuhojiwa kwa kina wameamua kumuachia kwa dhamana hata hivyo uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tuhuma hizo na upo uwezekano wa kumfikisha mahakamani.
Lijualikali, Suzan Kiwanga ambaye ni mbunge wa Kilombero na wenzao 55 jana (Desemba 21) walifika mahakamani hapo ambapo wanashtakiwa kwa makosa nane likiwemo la kuchoma moto ofisi ya kijiji cha Sofi Malinyi Oktoba 26 mwaka huu.
Hii ni awamu ya pili Lijualikali kufikishwa mahakamani ambapo awamu ya kwanza alifikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Kilombero kwa kosa la kufanya vurugu na baada ya kutiwa hatiani alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita.