Jumla ya mabasi 18 yamekamatwa kwa siku mbili mkoani Tanga kwa makosa ya kuzidisha nauli kwa abiria katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya baada ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa nchi Kavu na Majini (Sumatra) kwa kushirikiana na jeshi la polisi kuendesha msako maalumu.
Ofisa wa Sumatra mkoa wa Tanga Dk Walukani Luhamba alisema jana kuwa idadi hiyo ya mabasi ilikamatwa kufuatia kufanyika oparesheni iliendeshwa kwa siku mbili kwa lengo la kudhibiti vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wenye mabasi kupandisha nauli katika kipindi hiki cha siku kuu za Krismasi na mwaka mpya.
Amesema mabasi yaliyokamatwa katika oparesheni hiyo ni yale yaliyokuwa yakitokea Tanga kuelekea Dar es salaam , Mbeya, Moshi, Arusha, Dodoma na Morogoro na nchi jirani ya Kenya ambapo mbali ya kuongeza nauli, mengine yalikutwa na makosa ya abiria kutofunga mikanda, mikanda mibovu, na kuzidisha idadi ya abiria kama kulingana na maelekezo ya leseni husika.
“Tumeweka kambi katika barabara kuu eneo la Mkata, Segera, Korogwe na Mombo, hakuna basi litakaloruhusiwa kuendelea na safari, tutawashusha abiria na dereva tutamfikisha mahakamani lakini mmiliki atatozwa faini ya Sh300,000”alisema Dk Walukani.
Ofisa huyo amesema operesheni hiyo pia itahusisha ukaguzi wa mabasi yanayoondoka jijini Tanga kabla ya saa 12.00 alfajiri kwa sababu ni kinyume cha sheria ya usafirishaji wa abiria.
Hatua hiyo ya Sumatra, imepongezwa na wasafiri waliozungumza na Mwananchi katika kituo kikuu cha mabasi cha Kange Jijini Tanga waliosema kwa kipindi hiki kuna haja ya kuwadhibiti wenye mabasi kwani wanadai ni kipindi chao cha mavuno.
Flora Jonathani aliyesafiri kutoka Dar es salaam hadi Tanga jana amesema ameshuhudia abiria waliokuwa wakielekea Mkoani Kilimanjaro wakitozwa Sh40,000 kila mmoja ili kuweza kupata nafasi kwenye mabasi.
“Kwenye tiketi wanaandika nauli inayoruhusiwa na Sumatra lakini fedha halisi wanazotoa abiria ni kubwa mno na wanakubali ili waweze kupata usafiri kwenda kwao”amesema Flora.