MSHAMBULIAJI wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Elius Maguli, amesema kuwa maslahi bora na kutaka kujifunza changamoto mpya, ndiyo sababu kuu zilizomfanya "aukache" mkataba wa kujiunga na Yanga na kuichagua Polokwane City inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Maguli amebakiza miezi sita katika mkataba wake na Dhofar FC ya Oman, lakini ana ruhusa ya kujiunga na timu nyingine ambayo atafikia makubaliano nayo na kuhama bila ya kulipa ada yoyote ya uhamisho.
Akizungumza na Nipashe jana mjini hapa, Maguli, alisema kuwa mbali na Yanga, Simba za Tanzania zinazodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, pia alipata ofa za kujiunga na klabu nyingine za Oman, lakini Polokwane City ndiyo imefikia katika maslahi ambayo yatamsaidia kumuendeleza kimaisha na kipaji chake.
Maguli alisema kuwa anaamini atakapotua Afrika Kusini, atajifunza vitu vipya ambavyo hakuwahi kuvijua alipokuwa akicheza Tanzania na Oman na itakuwa ni mwendelezo wa safari yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya Afrika.
"Siwezi kusema au kuzungumza vibaya kuhusu Yanga au Simba ambayo niliwahi kuitumikia, lakini ni lazima pia niangalie maslahi yangu wapi watanilipa vizuri, maslahi ni kitu kikubwa kwa sababu mimi nina familia inayohitaji kupata matunzo bora," alisema Maguli ambaye ni baba wa watoto watatu wa kike.
Alisema kuwa mazungumzo yake na Polokwane City yako katika hatua ya mwisho na anatarajia kusaini mkataba wa miaka miwili huku akikataa kuweka wazi dau atakalokwenda kupokea na lile ambalo aliahidiwa na klabu za Tanzania.
"Kuhusu Polokwane City, sio tetesi, kwa sasa mimi ni mchezaji wao kwa asilimia 90, ninajiandaa kwenda kukabiliana na changamoto mpya," alisema Maguli ambaye aliwahi kucheza Tanzania Prisons ya Mbeya, Ruvu Shootinga (Pwani), Simba (Dar es Salaam), Stand United (Shinyanga) na Dhofar FC ya Oman.
Mshambuliaji huyo ambaye leo anatarajiwa kuiongoza Kilimanjaro Stars katika mechi ya Kombe la Chalenji dhidi ya Zanzibar Heroes, aliwataka wachezaji wa Tanzania kuwa na malengo na kuwaasa wale wanaopata nafasi ya kucheza nje kujituma zaidi ili kuitangaza nchi.