Mambo Yazidi Kuwa Magumu Bunge la Afrika Mashariki
0
December 22, 2017
Katika hali inayozidi kuleta mkanganyiko kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala), wabunge wawili wamechaguliwa wajumbe wa Tume ya bunge bila ya ridhaa yao.
Wabunge hao ni Fancy Nkuhi na Mariam Ussi Yahya ambao Jumatano Desemba 20,2017 walichaguliwa wajumbe wa tume licha ya umoja wa wabunge wa Tanzania katika Eala kutaka majina yao yaondolewe.
Kila mmoja alipata kura 35 katika uchaguzi uliosusiwa na wabunge wote kutoka Burundi.
Habari kutoka ndani ya Bunge zilizothibitishwa na msemaji wa Eala, Bobi Odiko zimesema wabunge wa Tanzania sasa ni wajumbe halali wa Tume licha ya Taifa hili kususia vikao tangu Jumatatu wiki hii.
Taarifa kutoka Eala zinasema wabunge hao walichaguliwa kwa kishindo kuwa wajumbe katika kikao kilichofanyika Jumatano ambacho kilihudhuriwa na wabunge watatu tu kutoka Tanzania.
Odiko alisema ni kweli umoja wa wabunge wa Tanzania ulishamwandikia barua Katibu wa Bunge la Eala mapema wiki hii kuwa majina ya Nkuhi na Yahya yaondolewe katika orodha ya wagombea ujumbe wa Tume ya Eala.
Hata hivyo, alisema ilipofika siku ya uchaguzi wagombea hao walikuwa hawajaondoa majina yao kutokana na utaratibu na ndipo walipochaguliwa kuwa wajumbe wa Tume ambayo kazi yake kubwa ni kuratibu shughuli za Bunge.
"Licha ya Tanzania kususia vikao vya Eala tangu Jumatatu baada ya kukapishwa, kulikuwa na wabunge wasiopungua watatu wakati wa uchaguzi wa wajumbe wa Tume," amesema Odiko.
Wabunge wa Eala kutoka Tanzania na Burundi wamekuwa wakisusia vikao vya Bunge kutokana na utata juu ya uchaguzi wa Spika.
Martin Ngoga alichaguliwa kuwa Spika baada ya vuta nikuvute. Wabunge kutoka Tanzania na Burundi walisusia uchaguzi huo kwa madai kuwa haikuwa zamu ya Rwanda kuteua mgombea.
Tags