Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kuwapo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
TMA iliyochini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema hayo katika taarifa ya utabiri wa hali ya hewa wa saa 24 zijazo uliotolewa leo Ijumaa.
Mamlaka hiyo imesema katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Shinyanga, Rukwa, Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera na Katavi kutakuwa na hali ya mawingu mvua na ngurumo katika baadhi ya maeneo na vipindi vifupi vya jua.
Imesema katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Songwe kutakuwa na hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vifupi vya jua.
Katika mikoa ya Iringa na Morogoro imesema kutakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Taarifa ya hali ya hewa imesema katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kutakuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua katika maeneo machache na vipindi vya jua.
Kwa mikoa ya Dodoma na Singida kutakuwa na hali ya mawingu kiasi na vipindi vya jua.
Kuhusu upepo wa Pwani TMA, imesema unatarajiwa kuvuma kutoka Kaskazini -Mashariki kwa kasi ya Km 30 kwa saa na kutoka Kusini -Mashariki kwa kasi ya Km 40 kwa saa kwa Pwani ya Kusini.
Mamlaka imesema kuhusu hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi hadi makubwa huku matazamio siku ya kesho Jumamosi kuwa na ongezeko la mvua maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini.