Akizungumza na gazeti hili jana, Mbowe alisema anasita kuweka bayana mikakati ya vyama vya Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa hofu ya kuitwa mchochezi.
Kwa mantiki hiyo ni kama Ukawa itaingia katika aina nyingine ya kufanya siasa baada ya ile iliyozoeleka kuwa ngumu kutokana na misukosuko wanayoipata.
Miongoni mwa viongozi wa upinzani wanaokabiliwa na kesi za uchochezi ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye ana kesi zaidi ya tano. Lissu kwa sasa yuko Nairobi nchini Kenya akitibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma.
Upinzani umekuwa na wakati mgumu tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 baada ya Rais John Magufuli kuzuia mikutano ya hadhara na viongozi wake kukamatwa mara kwa mara wakituhumiwa kwa uchochezi na wengine kufunguliwa kesi.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi baada ya gazeti hili kutaka kujua mwelekeo wa vyama hivyo baada ya kuwa kimya na kususia uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini utakaofanyika Januari 13 mwakani.
“Siwezi kutoa silaha zote hadharani maana nikisema watasema Mbowe mchochezi,” alisema kiongozi huyo wa upinzani bungeni.
“Na mtu anayefikiri haya tunayofanyiwa kuwa wanaoumia ni Chadema, anajidanganya. Upinzani makini unajenga Taifa imara.
“Kufanya kazi katika upinzani kwa awamu hii ni mateso. Haturuhusiwi kufanya mikutano ya kisiasa, haturuhusiwi kuendesha mijadala yaani unamfunga mikono nyuma halafu unamwambia njoo upigane.”
Wabunge wengine wanaokabiliwa na makosa ya uchochezi na baadhi kesi zao zimemalizika ni Halima Mdee (Kawe), Peter Lijualikali (Kilombelo), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini), Susan Kiwanga (Mlimba), Ester Bulaya (Bunda Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Saed Kubenea (Ubungo).
Kwa upande wa viongozi waliohojiwa au kufungulkiwa kesi wakihusishwa na uchochezi ni Dk Vincent Mashinji ambaye ni katibu mkuu wa Chadema, Edward Lowassa (waziri mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema) Patrick ole Sosopi (mwenyekiti wa Baraza la Vijana, Chadema), Salim Mwalimu (naibu katibu mkuu-Zanzibar) na viongozi wa ngazi ya mikoa, wilaya na kata.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kosa la uchochezi, wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia alisema wanasiasa watakuwa waathirika wakubwa kwa kuwa ni kosa la kisiasa.
“Ili kumaliza tatizo hili la uchochezi ni lazima tukubali uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa, lazima tuwe na Katiba Mpya,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu kutoweka wazi mikakati yao na ushiriki wa vyama hivyo katika uchaguzi wa marudio wa ubunge katika majimbo matatu utakaofanyika Januari 13, Mbowe alisema uamuzi huo hauwaumizi Chadema wala wapinzani, bali Taifa.
Vyama hivyo vimesusia uchaguzi vikidai kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ifanyie kazi changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 uliofanyika Novemba 26.
Katika uchaguzi huo uliotokana na baadhi ya madiwani kujiuzulu uanachama na kujivua nyadhifa zao kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais Magufuli, upinzani ulishinda kiti kimoja.
“Upinzani hautakufa ila utabadili operesheni. Hatuna sababu za kwenda kushiriki uchaguzi ambao watawala wameonyesha watashinda,” alisema Mbowe.
Alisema ni vigumu kuingia katika uchaguzi wakati tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, vyama vya upinzani vinabanwa na kuzuiwa kufanya siasa.
“CCM inatumia wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na mawaziri pamoja na vyombo vya umma huku sisi tukizuiwa. Wenzetu wanafanya mikutano, wanatumia vyombo vya habari vya umma, wanatumia ma- RC, DC, DED na mawaziri,” alisema.
“Wanasema tuje katika uchaguzi ambao imesikika kiongozi akisema ‘inawezekanaje unamtangaza mpinzani wakati nimekupa gari na nyumba’. Sasa watu wanataka ushahidi gani wa kuonyesha tunakandamizwa.”