Baada ya kuwepo kwa taarifa za kuhojiwa kwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenga, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi (61) na Idara ya Uhamiaji kuhusu uraia wake, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amesema utawala wa Rais Kikwete,makanisa yalisimama na kukosoa.
Heche amesema kwamba utawala wa Kikwete Kanisa lilisimama imara kukosoa mambo kadhaa ya serikali na wala hakuwahi kushuhudia viongozi wa dini wakihojiwa na kususitiza kwamba watu wasimame imara kupinga kuporwa kwa uhuru
"Kanisa lilisimama imara kukosoa mambo kadhaa wakati wa utawala wa Kikwete, sikuona kiongozi anahojiwa uraia wake naamini ingekuwa kipindi hiki kanisa lingefutwa wangesema sio kanisa la Kitanzania, tusimame imara kupinga uhuru wetu kuporwa, hakuna alie salama" Heche.
Taarifa zinadai kwamba Askofu Niwemugizi alihojiwa mara 2 na Idara ya Uhamiaji kuhusiana na Uraia wake kati ya mwezi Novemba na Disemba
“Mara ya kwanza niliitwa na kufika ofisi za uhamiaji Ngara, Novemba 28 na mara ya pili niliitwa Desemba 4.
“Niliombwa kibali kinachoniruhusu kuwa nchini, nikashangaa, nikasema mimi ni Mtanzania, nikaambiwa nilete document (nyaraka).
“Nilipeleka hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na cheti cha kuzaliwa, wakasema wataniita tena.
“Baada ya kuitwa mara ya pili, nilipewa fomu ya kujaza ambayo bado naendelea kuijaza hadi sasa.
“Waliniita tena wakasema bado wanataka kujiridhisha ndio maana wanataka nijaze fomu, ninaendelea kuifanyia kazi mpaka nitakapokuwa nimeikamilisha yote,” anasema Askofu Niwemugizi ambaye amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC).
Mwishoni mwa mwezi Septemba , Askofu Niwemugizi alisema kuwa imefika wakati nchi inahitaji kuwa na dira nzuri ambayo pia italetwa na Katiba Mpya .
Msemaji Mkuu Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda, amekiri askofu huyo kuhojiwa na kusema;
“Ni kweli anahojiwa na ofisi yetu ya Wilaya ya Ngara, ni suala tu la tuhuma si kwamba ni kweli au la, hivyo itakapothibitika basi itajulikana,” alisema Mtanda.