Meya wa Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Raymond Mboya amekanusha tetesi za kujivua wadhifa wake huo na kuhama chake cha Chadema na kuhamia CCM.
Mboya ambaye ni diwani wa Kata ya Longuo ametajwa kwamba ana lengo la kukihama chama hicho, lakini amekanusha na kusema kuhama chama na kuacha kazi sio kuunga mkono Serikali bali ni kuchezea rasilimali za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Desemba 27 ofisini kwake alisema, taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kutaka kuhama chama sio za kweli na wananchi wapuuze.
“Kila mmoja anaunga mkono Serikali lakini sio kwa kuacha kazi na kumuunga mkono mtu anayefanya kazi” amesema Mboya.
Alisema wanaofanya hivyo hawazitendei haki kazi ambazo wamepewa na wananchi hivyo wanatakiwa kuunga mkono kazi za Serikali kwa kufanya kazi ili kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema “ tumechaguliwa na wananchi ili tuwatumikie na sio wametuchagua ili tuharibu rasilimali”
Hata hivyo alisema katika kuunga mkono sera ya viwanda, manispaa hiyo inatarajia kuanzisha kiwanda kidogo cha mbolea inayotokana na takataka zinazolalishwa na wakazi wake.
Alisema kiwanda hicho ambacho kitaanzishwa kwa kushirikiana na serikali ya Ujerumani kitajengwa katika eneo la dampo kuu la takataka ambalo liko Kaloleni.
“Tunamuunga mkono Rais (Magufuli) katika suala la ujenzi wa viwanda na kweli juhudi zake zimetupendeza na tumeamua tutamuunga mkono mwezi Februari mwaka 2018, kwa kujenga kiwanda kipya cha kutengeneza mbolea eneo la Kaloleni…Tunasubiri barua rasmi ya uwekezaji wa mradi huo kutoka kwa wenzetu ambao ni mji dada wa Tübingen,” alisema.
Katika taarifa yake, Meya huyo alisema mwezi Januari, mwakani, Tubingen na Manispaa ya Moshi, watasaini makubaliano ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachotarajiwa kutumia malighafi ambayo ni takataka zinazokusanywa katika Manispaa ya Moshi.
Alisema kwa sasa wanajiandaa kwenda kutoa taarifa na kutambulisha mradi huo kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
Kwa mujibu wa Raymond, kila siku mji wa Moshi unazalisha taka, kati ya tani 180 hadi 200 na kwamba timu ya wataalamu wa ujenzi wa kiwanda hicho kutoka nchini Ujerumani, wameshakuja na kufanya tathmini na kujiridhisha malighafi hiyo inaweza kuendesha uzalishaji wa mbolea.
Ujenzi wa kiwanda hicho, unatokana na kukosekana kwa teknolojia ya kubadili taka ngumu zinazozalishwa na wakazi wa Manispaa ya Moshi ili zitumike kama nishati.