Gerald Deus (30), mkazi wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita aliyetoka jela kwa msamaha wa Rais, amehukumiwa tena kifungo cha miaka 15 jela.
Deus aliyehukumiwa kifungo hicho juzi na Mahakama ya Mwanzo Bukombe baada ya kukiri kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu, ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliopewa msamaha Desemba 9 na Rais John Magufuli.
Msamaha huo wa Rais ulitolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).
Deus alihukumiwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Bukombe, Damas Gakwaya baada ya kukiri kosa la kupora Sh300,000 kutoka kwa Dina Mwende, mfanyabiashara wa soda za jumla wilayani Bukombe.
Tukio hilo kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa Polisi, Mohamed Simai lilitokea katika Mtaa wa Malendeja, Kata ya Katente wilayani Bukombe saa sita mchana Desemba 14, ikiwa ni siku nne tu tangu mshtakiwa huyo atoke gerezani.
Simai aliiambia Mahakama kuwa kabla ya kupora kiasi hicho cha fedha, mshtakiwa alifika dukani akijifanya anataka kununua soda za jumla kwa ajili ya vibarua aliodai walikuwa wakilima shambani kwake.
“Wakati muuza soda akiendelea kupanga kreti dukani, ghafla mshtakiwa alimvamia na kumpora Sh300,000 na kuanza kutimua mbio kabla ya kukamatwa na raia wema waliojitokeza kutoa msaada baada ya kelele za aliyeporwa fedha,” Simai aliieleza Mahakama.
Mwendesha mashtaka alisema baada ya kumkamata, wananchi walianza kumshambulia lakini aliokolewa na polisi waliofika eneo la tukio. Baada ya kusomewa mashtaka, mshtakiwa Deus alikiri kutenda kosa hilo na kuiomba Mahakama imhurumie kwa kumpa adhabu ndogo kwa sababu ana siku tano tu tangu alipotoka gerezani kwa msamaha wa Rais Magufuli.
Akitoa hoja baada ya mshtakiwa kukiri kosa, mwendesha mashtaka aliiomba Mahakama kumpa Deus adhabu kali kwa sababu anaonekana ni mhalifu mzoefu na hajajifunza kwa kipindi cha miezi sita aliyokaa gerezani akitumikia kifungo cha mwaka mmoja alichohukumiwa kwa kosa la wizi.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Juni Mosi, mwaka huu, Deus alihukumiwa kifungo cha miezi 12 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la wizi wa nguo mali ya Naomi Musa, mkazi wa Mtaa wa Kapela, Kata ya Igulwa katika mji mdogo wa Ushirombo wilayani Bukombe.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mujuni Mchunguzi wa Mahakama ya Mwanzo Bukombe katika shauri la jinai namba 188/2017.
Kabla ya kutoka kwa msamaha wa Rais Desemba 9, mshtakiwa alikuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela katika Gereza la Kahama ambako ndiko alikorejeshwa juzi.
“Kwa sababu mshtakiwa amekiri kosa; na kwa kuzingatia ametenda kosa hilo siku chache tu baada ya kutoka Magereza kwa msamaha wa Rais; naiomba Mahakama kumpa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo,” aliomba Simai.
Akitoa hukumu, Hakimu Gakwaya aliyeonyesha mshangao kwa mshtakiwa kushindwa kutumia vizuri msamaha wa Rais Magufuli, alisema Mahakama inamhukumu kifungo cha miaka 15 jela badala ya miaka 30 aliyostahili kwa mujibu wa sheria kwa sababu hakuisumbua Mahakama kwa kukiri kosa.
“Kwa sababu hujaisumbua Mahakama kwa kukiri kosa; nakupa adhabu ya onyo ya miaka 15 na kazi ngumu gerezani ili iwe fundisho kwako na kwa wengine,” alisema hakimu Gakwaya.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 285 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 16 na marekebisho yake ya mwaka 2002.
Mfungwa Aliyesamehewa na Rais Magufuli Atupwa Jela Miaka 15
0
December 18, 2017
Tags