Matonya ndiye mfungwa mwenye umri mkubwa kuliko wote walioachiwa kwa msamaha wa Rais siku ya Uhuru, Desemba 9.
“Bado ninalo neno la kumwambia Rais (John) Magufuli kama nitakutana naye, lakini kama nitashindwa kumuona nitabaki na neno hilo moyoni mwangu, ila Watanzania wajue kuwa niliua kweli naomba Mungu anisamehe na wao wanisamehe pia.” Hayo ni maneno ya Mganga Matonya.
Matonya ndiye mfungwa mwenye umri mkubwa kuliko wote walioachiwa kwa msamaha wa Rais siku ya Uhuru, Desemba 9.
Matonya (85), ambaye ametoka Gereza la Mkono wa Simba mkoani Morogoro na kurudi kijijini kwao Wiliko, Wilaya ya Chamwino anasema hadi sasa anahisi kama anaota kwa kuwa hakuwahi hata siku moja kuwaza kuwa angetoka gerezani na kurudi uraiani.
Kijiji cha Wiliko kipo umbali wa kilomita 81 kutoka katikati ya Mji wa Dodoma katika barabara ya kuelekea Iringa, kijiji hicho kipo mwishoni mwa wilaya hiyo jirani na Jimbo la Isimani mkoani Iringa.
Matonya ni nani
Mganga Matonya ‘Chigoma’ ni baba wa watoto sita, wajukuu 34 na vitukuu tisa ambao wanaishi kijijini hapo.
Matonya ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliopata msamaha wa Rais Magufuli, lakini akiwa mfungwa mzee kuliko wote huku akidumu gerezani kwa miaka 44 ambayo aliishi katika magereza ya Isanga (Dodoma) na Mkono wa Simba (Morogoro).
Kwanini alikwenda gerezani?
Tofauti na wengi ambao huzunguka pale wanapohisi kuwa wamekosea, Matonya anasema moja kwa moja kuwa, “niliua baada ya kuona mwenye mali analeta ugumu na mimi pamoja na wenzangu watatu tukachukua ng’ombe 12.”
“Nilikuwa na tabia ya wizi wa mifugo enzi hizo nikiwa kijana, maeneo mengi tuliiba, lakini siku hiyo ilikuwa mimi na rafiki yangu Muyeya Nyagalu ndugu zetu wa kabila la Masai wawili, tulikuta ng’ombe wale wazuri sana, lakini mwenye mifugo alikuwa mkali na kama tungekuwa watepetepe mmoja wetu angekufa hapo.
“Tulipomuua tuliondoka na mifugo na utaratibu huwa ni kugawana kila mtu anakwenda na mzigo wake, hapo ndipo kosa langu lilipotokea maana nilikwenda mnadani na nilikamatwa nikiwa na ng’ombe sita.”
Hata hivyo, anasema alipokamatwa mnadani, alifanikiwa kuwakimbia wakamataji na akarudi hadi nyumbani kwake, lakini siku tatu baadaye alishangaa kuona kundi la watu likiwa limezingira nyumba yake na wakati huo alikuwa juu ya nyumba yake ya tembe akiendelea kuezeka udongo kwa kuwa msimu wa mvua ulikuwa umekaribia.
Apelekwa Isanga
Tangu Oktoba 1974, Matonya ambaye alijulikana kwa jina la utani la Chigoma alikuwa katika mahabusu ya Gereza la Isanga, lakini miaka sita baadaye alihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, ushahidi usio na shaka uliwatia hatiani yeye na Nyagalu huku watu wengine waliokuwa wamekamatwa kwa makosa hayo wakiachiwa huru na wale ndugu zao wa kabila la Masai hawakuonekana hata kwenye kesi.
Kabla ya kueleza mengi, anakiri kuwa wapo watu waliofungwa magerezani kwa makosa ambayo hawakuyatenda lakini yeye alikuwa gerezani kwa kosa ambalo alilitenda.
Mzee huyo ambaye anarudia rudia maneno ya kuomba msamaha mbele za Mungu na wanadamu, anasema hukumu aliyopewa ilistahili kwa kuwa hata walipomuua mfugaji bado hakuona shaka kama damu ya mtu ilikuwa imemwagika bali aliwaza kupata mali.
Anasema katika hukumu hiyo ya mwaka 1983, alijua angenyongwa muda si mrefu na hivyo alikuwa amekata tamaa ya maisha na hakuwaza chochote zaidi ya kuagiza mkewe aende wakaonane na kumuaga.
“Kikubwa nilichokuwa nafanya mle gerezani ilikuwa ni kufanya kazi, kwa kweli mimi nimefanya kazi nyingi sana gerezani nilizotumwa na ambazo sikuwa nimetumwa, maana nilijua hiyo ndiyo sehemu ya kujiliwaza kwani ukifanya kazi ngumu unachoka na hivyo ukilala unapata usingizi,” anasimulia.
Abadilishiwa kifungo
Mzee Mganga anaukumbuka mwaka 1983 alipopelekewa taarifa na mkuu wa gereza ambaye amemsahau kwa jina kwamba Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa amemsamehe adhabu ya kunyongwa hadi kufa na kuwa kifungo cha maisha.
“Ndiyo maana nasema kama mtu akinipeleka kwenye kaburi la Nyerere ningeinama na kumshukuru sana mzee huyu, maana asingefuta adhabu ya kifo huenda huyu wa sasa (Magufuli) asingenikuta hai,” anasema Mganga.
Anasema katika fikra zake aliamini kuwa angeweza kuishi walau hata miaka mitano mbele, lakini tumaini la kurejea uraiani halikuwapo.
Baada ya kubadilishiwa adhabu hiyo, alikaa Gereza la Isanga kwa mwaka mmoja kisha akapelekwa Gereza la Mkono wa Simba mkoani Morogoro ambako alikaa kwa miaka 33.
Maisha ya gerezani
Mzee huyo mchangamfu anasema maisha ya gerezani ni ya tabu na kukatisha tamaa.
“Kule hakufai, hakuna uhuru, hakuna masikilizano yaani kuna utofauti mkubwa na huku uraiani. Hata hivyo askari magereza wanafanya kazi ngumu sana maana mchanganyiko wa watu una shida kwa ujumla,” anasema mzee Matonya.
Anasema gerezani hakuna upendo na busara zake ndani ya gereza ndizo zilimpa nafasi nyingi za kuongoza wenzake na kuwasimamia mpaka ukafika wakati akaona walau ugumu wa maisha unapungua.
Hata hivyo, anasema katika maisha yake gerezani alikuwa mfano mzuri wa kuchapa kazi.
Nini anakikumbuka gerezani?
“Siwezi kukumbuka kitu mle ndani zaidi ya kuwaombea ndugu na vijana wangu niliowaacha mle ambao wengi naamini itawachukua muda mrefu kurudi uraiani,” anasema.
Kingine anachokumbuka ni namna ambavyo mkewe na watoto walivyokuwa wakimtembelea mara kwa mara akiwa Isanga, lakini anataja ugumu wa maisha kuwa uliifanya familia yake ishindwe kwenda mara nyingi mkoani Morogoro.
Anakumbuka mke wake alikwenda mara moja mkoani humo katika kipindi cha miaka 33, huku mtoto wake mkubwa akifika mara mbili na mkewe lakini mwanawe wa tatu alikwenda mara nyingi zaidi na familia yake.
Kitu gani anatamani maishani?
Kwa sasa Mganga anatamani kupata nafasi ya kuwa mshauri wa vijana na watu wenye tabia za wizi na udokozi, akisema kuwa hazilipi hata kidogo zaidi ya kuwarudisha nyuma.
Kazi hiyo alikuwa akiifanya tangu alipokuwa gerezani na anasema baadhi ya watu aliokuwa akiwapa ushauri huko walikuwa wakirudi uraiani wanakuwa raia wema kiasi cha kumtembelea gerezani kwa ajili ya kumshukuru.
Ombi lake jingine ni kwa jamii pamoja na Serikali kumuonea huruma na kumwezesha walau kitu chochote cha kuanzia maisha na mkewe ambaye anasema kwamba alikuwa mvumilivu wakati wote, licha ya kuzaa watoto watatu nje ya ndoa yao lakini bado aliwaandika kuwa katika ukoo wake na alivumilia kuishi na familia yake hadi mwisho.
Anasema kwamba hawezi kurudia kosa la aina yoyote zaidi ya kuishi kwa kumtegemea Mungu na kujikita katika kilimo ili mvua zikinyesha apate chakula cha familia yake.
Alipataje taarifa ya kuachiwa?
Anasema siku ya sherehe za uhuru akiwa na wenzake na kwa sababu ya umri wake alikuwa amelala kivulini, huku wafungwa wengine wakisikiliza na kuangalia televisheni.
Anaeleza kuwa ghafla mfungwa mwenzake anayemtaja kwa jina moja la Mlyuka mwenyeji wa mkoa wa Njombe alimfuata na kumwambia kuwa majina yao yametajwa kwamba wamesamehewa.
“Nilimuuliza Mlyuka kama ni kweli akasema ni kweli tumetajwa,” anasema mzee Mganga na kuongeza kuwa baadaye wafungwa wenzake waliwapongeza kabla ya askari wa gereza kuwaita na kuwaambia wajiandae ili siku inayofuata waruhusiwe.
Mabadiliko anayoyaona
Kutokana na kuishi muda mrefu gerezani, anasema hata kijiji chake anaona si kile alichokiacha zaidi akikumbuka miti mikubwa michache aliyoiacha.
Kwa mujibu wa mzee huyo hata jua anaona linatokea upande ambao halikuwa likitokea na wakati mwingine anahisi kuwa hayuko katika dunia ya sasa.
Mzee Matonya anafurahi kuwa anaongea na watu kwa uhuru mpana tofauti na wakati ambao alikuwa anaongea na nduguze akiwa gerezani kwa kuhesabiwa dakika,.
Jambo jingine lisilomfurahisha ni namna ambavyo mazingira yameharibiwa zaidi kijijini kwao huku idadi ya watu wakiongezeka na majumba kuwa mengi.
Simulizi ya watoto
Kwa mujibu wa mtoto wa pili wa mzee huyo aitwaye Jeremiah Mganga, baba yake alikamatwa wakati yeye akiwa na miaka mitano na tangu wakati huo maisha yao yalikuwa magumu.
Jeremiah mwenye mke, watoto watatu na wajukuu watatu anasema wakati wote baba yao alikuwa akiwaagiza yeye na wadogo zake kwenda na mama yao katika Gereza la Isanga.
Anasema siku ya kukamatwa kwa baba yake alikuwa nyumbani kwao anacheza nje na mama yake, ndipo ghafla akaona watu wengi baadhi wakiwa wamevalia kofia, lakini kwa umri wake alijua ni ndugu waliokwenda kumchukua baba kwa ajili ya mambo yao.
Jeremiah anasema kuwa mama yake mzazi ndiye aliyepata wakati mgumu zaidi kwa kuwa alikuwa akitengwa sana na jamii kijijini na hata yeye (Jeremiah) aliona kila kitu hadi alipokuwa mtu mzima.
Anasema aliamua kuihamisha familia yao kutoka mahali alipowaacha baba yao na kwenda katika kitongoji kingine ndani ya kijiji hicho. “Lakini namshukuru sana mdogo wangu huyu Aron (anamuonyesha), mwenzetu alikuwa anakwenda mara kwa mara Morogoro na kutuletea taarifa za huko na alikwenda na familia yake mara kadhaa ndipo nasi tulikwenda mara mbili,” anasema.
Kwa sasa hana hofu juu ya maisha ya baba yake kwamba kurudi kwake hakuwezi kuhatarisha maisha kwa kuwa anaamini tukio lililomfanya afungwe ni la muda mrefu na hata familia ambayo ndugu yao aliuawa watakuwa wamewasamehe.
Kwa upande wake, Aron ambaye baba yake alimuacha akiwa bado tumboni mwa mama yake, anasema alikuwa akipata shida kuishi mbali na mzazi wake huyo na alianza kumfahamu akiwa gerezani.
“(Wakati yupo) Isanga nilikuwa bado mdogo, lakini nilipomaliza shule ya msingi nilitumia nguvu kubwa kumtafuta hadi nikamuona alipo, ndipo nikawa nakwenda mara kwa mara mimi na mke wangu pamoja na watoto wangu watatu,” anasema.
Aron anasema awali kaka yake aliwahi kuuza ng’ombe watatu ili amtafute baba yake gereza alilokuwa baada ya kuambiwa kuwa hayupo Isanga, lakini walishindwa hadi fedha ziliisha kabla ya yeye kumuibua mwaka 1997.
Anasema kabla ya kuachiwa kwa msamaha wa Rais, alitumia kila njia kuona baba yake anarudi uraiani lakini alishindwa na kwamba, alishangaa Desemba 9 akipigiwa simu kuambiwa kuwa jina la baba yao lilitajwa.
Aron anasema kama baba yake angekuwa nyumbani tangu 1974 na akajikita zaidi katika kilimo, maisha ya familia hiyo yangekuwa mazuri na yenye mafanikio kiuchumi.
Majirani wanamzungumziaje?
Victoria Ulaya (87) ambaye walikuwa majirani tangu wakati huo, anasema hakuwahi kujua kama Matonya ni mwizi wa mifugo kwa kuwa tabia hiyo hakuionyesha katika maeneo yao.
Anasema hata siku ya kukamatwa kwake wengi walionyesha mshangao kuona kumbe ndiyo kitu alichokuwa anakitegemea.
Victoria anasema kwamba siku alipokamatwa Matonya kundi la watu lilifika nyumbani kwake kutaka kujua kilichomsibu, lakini hata matajiri wa ng’ombe walimtetea.
“Tulishangaa zaidi tuliposikia kuwa ameiba tena ameua, ha! Ni huyu Mganga? Wakasema ndiyo, tukafumba midomo kweli, lakini kabla ya hapo alikuwa ni mstaarabu aliyempenda mke wake kweli,” anasema jirani huyo.
Balozi wa nyumba kumi
Balozi wa mtaa anaoishi Matonya, Ainea Sendu anasema maisha ya familia hiyo ni mazuri na hakuna mtoto hata mmoja aliyezaliwa na mzee huyo mwenye tabia ya udokozi.
Sendu (49) anasema alianza kusikia habari za Matonya tangu akiwa mtoto na kuwasikia watu wakiimba nyimbo kwenye vilabu vya pombe zilizomtaja, lakini hakuwa na tumaini kwamba ipo siku atakuja kukutana naye.
Balozi huyo anasema kwa sasa wanashirikiana na familia hiyo ili kutengeneza utaratibu wa kwenda kumshukuru Mungu kanisani.
Sendu anasema kwamba anakusudia kupeleka wazo kwa uongozi wa kijiji ili wamfanye mzee huyo kuwa mmoja wa wazee washauri.
Kiongozi huyo wa mtaa anasema sasa katika makazi ya Matonya ni kama kuna kituo cha utalii kwa kuwa idadi ya watu wanaofika eneo hilo ni kubwa zaidi kuliko maeneo mengine na wengi wanashinda hapo, huku wakimsikiliza mzee huyo ambaye wakati wote anaonyesha kujutia kosa alilofanya