Hatua ya vituo vya televisheni nchini hususan ya Taifa (TBC) kurusha moja kwa moja matukio na mikutano inayowahusisha viongozi wa Serikali na CCM, imeibua mjadala miongoni mwa jamii.
Katika mjadala, wapo waliogusia kuzuiwa kuonyeshwa mijadala ya Bunge moja kwa moja (live), kwa kigezo cha kuelemewa gharama na kubainisha kuwa kama viongozi hao wanaonyeshwa, hata vipindi vya Bunge vinapaswa kuonyeshwa kama ilivyokuwa zamani.
Wakati baadhi yao wakidai matangazo hayo yanalenga kuwazima viongozi wasio wa Serikali na vyama vya upinzani wanaokosa nafasi za kuonekana moja kwa moja, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi ametoa ufafanuzi akibainisha kuwa katika matukio ya kitaifa, vituo vya televisheni huombwa kurusha matangazo hayo.
Alisema, “Hivi ni TBC tu? Televisheni zote zenye uwezo wa kuonyesha huwa zinaonyesha. Suala la TBC kuzidi au kutozidi hiyo si hoja. Mfano mkutano mkuu wa CCM, televisheni nyingi zilionyesha.”
Dk Abbasi alisema katika matukio ya kitaifa, akitoa mfano wa maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, pia huwa vivyo hivyo.
Katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Desemba 17, mjini Dodoma, vituo kadhaa ikiwamo TBC viliuonyesha moja kwa moja kuanzia asubuhi hadi jioni.
“Kuhusu matukio mengine kuonyeshwa, hapo uziulize hizo televisheni zenyewe zitakuwa na majibu. Mimi nasimamia maonyesho ya kitaifa,” alisema.
Dk Abbasi alisema ikitokea Waziri Mkuu akaenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuzindua kitu halafu televisheni ikaonyesha tukio hilo, huenda kukawa na makubaliano kati ya televisheni husika na benki.
“Wakati mwingine tatizo si kuonyesha, pia mtazame mhusika mkuu wa tukio hilo ni nani,” alisema.
Januari mwaka jana, Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Nape Nnauye ilitangaza kuzuia kuonyeshwa moja kwa moja matangazo ya mijadala ya Bunge ikieleza kuelemewa na gharama ambazo TBC inalipia.
Nape alitoa sababu nyingine ya kusitisha matangazo hayo wakati wa Bunge la 10 kuwa ni mpango wa Serikali kuanzisha studio yake.
Alisema Serikali ilikuwa ikitumia Sh4.2 bilioni kurusha mikutano minne ya Bunge kwa mwaka. Kwamba shirika hilo limekuwa likigharamia kwa sehemu kubwa kulipia matangazo hayo kwa kutumia matangazo madogo ya biashara.
Alisema asilimia 75 ya vipindi vya TBC hutumika kutoa elimu kwa umma na asilimia 25 ni burudani hivyo, TBC iliona ni vyema kubadilisha mfumo ili kukabiliana na kuzidi kupanda kwa gharama za uendeshaji.
Ingawa hatua hiyo ilipingwa na wabunge wa upinzani na mashirika ya haki za binadamu, Serikali ilishikilia msimamo wake na kufafanua ni kwa nini ilifikia uamuzi huo.
Ni kama maelezo hayo hayajakata kiu kwani kina linapoibuka suala linalohusu kurusha matangazo ye televisheni live, suala hilo limekuwa likijirudia.
“Sijui kama wahusika wanalipia au la, hasa katika chombo cha habari cha umma,” alisema Dk Onesmo Kyauke wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) katika maoni yake.
“Nadhani vyama vyote vya siasa vipo sawa na tulishuhudia katika kampeni za uchaguzi mwaka 2015 vyama vingi vilionyesha matangazo yake moja kwa moja. Jambo hili likifanyika katika televisheni binafsi huwezi kuhoji sana ila televisheni ya Taifa yatasemwa mengi, ni lazima ulipe.”
Dk Kyauke aligusia mikutano ya Bunge, akisema umefika wakati wa kuruhusu ionyeshwe moja kwa moja ili wananchi kushuhudia wawakilishi wao wanachokifanya bungeni.
Mtazamo wa Profesa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Mwesiga Baregu ni kwamba kuongezeka kwa matukio hayo kuonyeshwa moja kwa moja kuna lengo la kuwazima wengine akitoa mfano wa viongozi wa vyama vya siasa.
“Unaweza kujiuliza ni kwa nini wazuie matangazo ya Bunge, kwa nini wao ndio waonekane kila siku...? Viongozi waliopita walijitahidi kutenganisha shughuli za chama na Serikali,” alisema Profesa Baregu ambaye pia mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Alisema, “Ni kutaka kuonekana zaidi tu kuliko wengine, huwezi kusema mtumishi wa umma amsikilize na kumheshimu mwanachama wa CCM, sasa siku chama hiki kikitoka madarakani itakuwaje?”
Mhadhiri wa uandishi wa habari na mawasiliano ya umma wa Chuo Kikuu Tumaini, Kizzito Noya alisema, “Kurushwa ‘live’ matangazo inategemea na tukio husika. Huwa hairuhusiwi kurusha muda mrefu tukio ambalo halina masilahi kwa umma, “Hairuhusiwi kurusha matangazo kwa masilahi ya mtu mwenye pesa maana unawanyima watu wengine demokrasia na uhuru wa habari,” alisema.
“Mfano katika gazeti, matangazo yanatakiwa kutozidi asilimia 60, hata katika televisheni pia ni vivyo hivyo. Mfano kuruhusu mtu alipie pesa kuonyesha harusi yake kwa saa zaidi ya tatu. Hii si sawa.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Gaudence Mpangala aliungana na Profesa Baregu na kufafanua kuwa huenda kuna mkakati wa kuimarisha jambo fulani kutokana na matukio ya urushwaji matangazo moja kwa moja kuongezeka.
“Mikutano ya Bunge lenye wawakilishi wa wananchi halionyeshwi live lakini matukio mengine, hata ya chama tu yanaonyeshwa moja kwa moja.”