Moshi Pafulika Yaelemewa na Wageni

Moshi Pafulika Yaelemewa na Wageni
Mikate jana asubuhi iligeuka bidhaa adimu katika maduka makubwa mjini hapa, kutokana na wingi wa wateja uliosababishwa na utamaduni wa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka walikozaliwa.

Mbali ya wingi wa wageni waliorejea kusherehekea sikukuu, msongamano wa magari katikati ya mji na barabara ya njia panda ya Himo-Moshi jioni unaonekana kuvunja rekodi.

Maduka makubwa ya bidhaa (supermarkets), jana asubuhi yalikuwa hayana mikate kutokana na mingi kununuliwa juzi na wenyeji wanaoenda vijijini kwa ajili ya sikukuu.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kati ya saa mbili asubuhi hadi saa nne uliobaini upungufu wa mikate na wasambazaji walichelewa kuisambaza.

Katika baadhi ya maeneo mikate iliyokuwepo ni iliyokaa dukani kwa zaidi ya siku mbili.

“Hatuna kabisa mikate, ilimalizika jana (juzi) usiku kwenye saa tatu. Wateja walikuwa wengi na kila mmoja alinunua mkate mmoja au miwili kwa ajili ya kwenda nayo kijijini,” alisema mhudumu mmoja.

Katika maduka hayo, bidhaa nyingine iliyonunuliwa kwa wingi ni bia na pombe kali.

Vilevile kulikuwa na misururu mirefu ya wateja wakinunua bidhaa hizo na kupakia kwenye magari. Wateja pia walikuwa wengi kwenye masoko ya Mbuyuni na Kati.

Mji wa Moshi kwa siku tatu mfululizo hadi jana umeonekana kuelemewa na wingi wa magari.

Barabara Kuu ya Dar es Salaam -Moshi, ndiyo iliyotia fora kwa msongamano wa magari kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa tatu usiku. Nyingine iliyokuwa na msongamano ni ya kutoka stendi kuu hadi mzunguko wa magari wa YMCA.

Kutokana na msongamano huo, magari yalikuwa yakitumia hadi dakika 40 kutoka eneo la Stop and Shop karibu na Kiboriloni hadi katikati ya mji, wakati kwa siku za kawaida huchukua kati ya dakika tatu hadi tano.

Msongamano pia ulikuwepo barabara lilipo Kanisa Katoliki la Kristo Mfalme hadi masoko ya Mbuyuni na Kati na barabara ya kuelekea Arusha.

Askari wa usalama barabarani wamejikuta katika wakati mgumu wa kuongoza magari kuanzia barabara ya Polisi Majengo, mzunguko wa magari wa YMCA na soko la Mbuyuni.

Gazeti hili lilishuhudia waendesha pikipiki maarufu bodaboda wakihusika katika ajali wengi kwa kugonga magari kwa nyuma ikidaiwa hilo linachangiwa na kutokuwa wazoefu wa foleni kama ilivyo jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro anayeishi Dar es Salaam ambaye jana alikuwa kijijini kwao Mwika, Moshi Vijijini, William Shao alisema kwa sasa kinachoendelea ni masuala ya kunywa na kula.

“Huku ni sherehe tu tunakula na kunywa, tena kuna ile Mbege (pombe ya asili kwa Wachaga) original (halisi) kabisa. Ni ndafu, mbege na kula. Huu ni utamaduni mzuri sana,” alisema Shao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad