LICHA ya kutua Ndanda FC, kiungo mshambuliaji Mrisho Ngassa amepanga kurejea kwenye timu hiyo kwa ajili ya kudai malipo yake ya mshahara.
Kiungo huyo, amejiunga na Ndanda hivi karibuni katika usajili wa dirisha dogo lililofungwa Ijumaa iliyopita.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ngassa alisema hajaachwa kama watu wanavyosema, isipokuwa mkataba wake Mbeya City ulimalizika.
Ngassa alisema, anashukuru ameondoka kwa amani katika timu hiyo na kikubwa amepanga kurejea katika timu hiyo kwa kudai malimbikizo yake ya fedha ikiwemo mshahara wake.
Aliongeza kuwa, hivi sasa anajiandaa kwa ajili ya kwenda kukutana na changamoto mpya katika timu yake ya Ndanda katika mzunguko wa pili wa ligi kuu.
“Ni jambo jema kwangu kuondoka kwa amani kabisa Mbeya City na ninashukuru nimemalizana nao salama mara baada ya mkataba wangu wa miezi sita kumalizika.
“Lakini nikiwa naenda zangu Ndanda kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo, nimepanga kurejea tena Mbeya kwa ajili ya kudai malimbikizo ya fedha zangu ikiwemo mshahara.
“Na ninashukuru viongozi wa Mbeya wamenihakikishia kunipatia fedha zangu hizo hivi karibuni mara baada ya kuwapatia taarifa za fedha zangu,” alisema Ngassa.