Wanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha jana walishindwa kuhudhuria ibada maalumu kwa sababu ya msiba wa ndugu yao Chimbuza Chrizoo uliotokea Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) wiki iliyopita.
Chrizoo alifariki dunia nchini humo, akiwa usingizini baada ya kumalizika kwa sherehe za kupongeza kuachiwa huru kwa familia ya Nguza.
Ibada hiyo iliyoandaliwa katika Kanisa la Life in Christ Ministries Zoe, lililopo Tabata Segerea jijini Dar es Salaam, ilikuwa na lengo la wanamuziki hao kumshukuru Mungu na Rais John Magufuli kwa kuachiwa huru Desemba 9.
Babu Seya na Papii Kocha walikaa gerezani miaka 13 na miezi minne wakikabiliwa kosa la kubaka na kulawiti watoto 10 wa kike ambao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.
Hii ingekuwa mara ya pili kwa wanamuziki hao kwenda kanisa hilo, kwani mara ya kwanza ilikuwa Desemba 9 muda mfupi baada ya kutoka gereza la Ukonga, walikwenda kanisani hapo na kuombewa na Nabii Joseph takriban saa tano.
Jana, akiwa katikati ya ibada, Nabii Joseph alisema: “Natambua uwapo wa waandishi wa habari ambao wamekuja kanisani hapa, kuchukua taarifa za Babu Seya na Papii Kocha. Hata nyinyi waumini mnataka kujua hii taarifa si ndiyo.
“Ni kweli Babu Seya na Papii Kocha walitakiwa kuja leo (jana) hapa kwa ajili ya maombi ya kumshukuru Mungu na Rais Magufuli, lakini kutokana na msiba wa ndugu yao nimeona ni vyema wakapumzika kwa ajili kupata faraja na upendo na wameniambia ni nikusalimieni sana,” alisema Nabii Joseph na kupigiwa makofi.
Aliwahakikisha waumini hao na wanahabari kuwa Jumapili ya wiki hii familia ya Nguza itakuwapo kwenye kanisa hilo na watazumgumzo masuala mbalimbali ya Mungu.
Alisisitiza siku hiyo itakuwa ya faraja na kuwataka waumini kujitokeza kwa wingi kwenye ibada hiyo maalumu itakayomuombea pia Rais Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Ratiba itakuwa ni hivi ataanza kuzungumza Michael Nguza, atafuata Babu Seya na wa mwisho atakuwa ni Papii Kocha kisha wataimba wimbo maalumu nilioutunga,” alisema.