Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amesema klabu yao haijapokea barua rasmi kutoka uongozi wa klabu ya AFC Leopards ya Kenya kumtaka beki wa kushoto wa Yanga Mwinyi Haji ambaye alifanya vizuri akiwa na kikosi cha Zanzibar Heroes kwenye mashindano ya CECAFA Senior Challenge Cup 2017 yaliyomalizika hivi karibuni nchini Kenya.
Mkwasa amethibitisha kupokea simu kutoka uongozi wa AFC Leopards lakini alipowaambia waandike barua rasmi ya kutaka kumsajili Mwinyi bado hawajafanya hivyo hadi sasa.
“Nilipokea simu kutoka kwa viongozi wa AFC Leopards lakini kiutaratibu nikawaambia watuletee barua rasmi kama wana nia ya kumtaka mchezaji ili sisi tuweze kuzungumza na mchezaji kwa ajili ya taratibu za uhamisho lakini hadi sasa hatujapata barua kutoka kwao, tumepata barua kutoka kwa mchezaji akitaka kuondoka kitu ambacho ni nje ya utaratibu”-Charles Boniface Mkwasa
“Hatumzuii mtu, sera yetu haizuii mchezaji kuondoka Yanga, Msuva alikuwa mchezaji mzuri sana kwetu lakini kwa sababu ilikuja klabu inamtaka na sisi tukaangalia kwa faida ya maendeleo yake na taifa tukamwachia akeenda Morocco sisi tumebaki tunapambana.”
“Mchezaji anapopata fursa tunamruhusu aende kwa sababu anafungua milango kwa wengine lakini hatujapata barua rasmi kutoka kwa AFC Leopards.”
Siku za hivi karibuni Mwinyi aliandika barua kwa uongozi wa klabu yake akiomba amwachie akatafute maisha sehemu nyingine kufuatia kuwekwa benchi kwa muda mrefu huku akiwa fiti na akiamini bado ana uwezo wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha Yanga.