Mtulia Apingwa Kila Kona Baada ya Kutangaza Nia ya Kugombea Ubunge Kinondoni

Mtulia Apingwa Kila Kona Baada ya Kutangaza Nia ya Kugombea Ubunge Kinondoni
Uamuzi wa aliyekuwa mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia kuhamia CCM na kutangaza nia ya kutaka kuomba ridhaa ya kuwania tena ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama tawala umepokewa kwa hisia tofauti huku wengi wakimponda katika mitandao ya kijamii.

Japokuwa wapo waliompongeza kwa hatua hiyo na pia uamuzi wake huobaada ya kueleza nia yake hiyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, wengi wameonekana kukerwa huku wakisema hataweza kushinda tena.

Desemba 2, Mtulia alijiuzulu ubunge baada ya kubaini kuwa Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani yake na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani uliahidi kuyatekeleza.

Kupitia ujumbe wake Facebook, Mtulia aliwapa pole wananchi wa jimbo hilo kwa maumivu waliyoyapata kwa uamuzi wake wa kujiuzulu ubunge.

“Nawahakikishia bado ninawapenda nipo tayari kuwatumikia tena kwa lengo la kuleta maendeleo kwenye jimbo letu. Nichukie fursa hii kutangaza nia kwa wana Kinondoni wote na Watanzania kwa ujumla kuwa nitachukua fomu ya kuomba ridhaa kwenye chama changu cha CCM,” alisema.

“Endapo chama changu kitaridhia, basi nitakuja mbele yenu kuomba ridhaa ya kuwatumikia katika nafasi ya ubunge wa jimbo letu Kinondoni.” Baada ya andiko hilo, mwananchi aliyejitaja kwa jina moja la Benson katika ukurasa wa Facebook ameandika, “...Naamini unaposoma ujumbe wa watu moyo unakusuta, najua unagombana na nafsi yako ukiwa umekaa peke yako.”

Pia, kupitia ukurasa wa mbunge huyo wa zamani, mmoja wa wafuasi wake, Dulla wa Mzumbe aliandika, “Watu walikuwa wakipigwa ili washinikize utangazwe nafasi ya ubunge, leo umekuwa kibaraka wa CCM huna lolote na ubunge hupati tena maishani mwako.”

Adam Nigangwa alisema, “... Kwanza CCM wenyewe wataanza kukugwaya, sasa hivi wanakuona kama karatasi la kufungia vitumbua.”

Bosco Mfundo amesema, “... Laana ya wana Kinondoni haitakuacha salama.”

Abdallah Kayela ameandika, “Jamani si ndio huyu aliyeapa kupitia kitabu cha Mungu pale kwenye ukumbi wa sokoni Tandale kuwa yeye si CCM na hawezi kuwa CCM mpaka kufa, Braza akili ya kuambiwa changanya na zako hela ulizopata tafuta biashara ufanye.”

Katika maoni yake, John Mazanda alisema Mtulia alichaguliwa kwa gharama kubwa, ikiwa ni pamoja na wananchi kukesha kulinda kura zake zisiibiwe na kwamba ni vyema angehama karibu na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Deus Mandara amesema, “Yaani umetuona wana Kinondoni ni malofa kiasi hicho! Ulikuwa hujulikani lakini Ukawa walikufanya watu wakujue... Rudi tena uone.”

Mohamed Lamimu ameandika, “...Kama moja ya ahadi ilikuwa kukufanya uwe mgombea tena wamekutapeli. Kama utakuwa mgombea basi labda watumie mabavu ili uwe mbunge.”

Mbali na kumshukia, wafuasi wake hao nao walikuwa wakitupiana vijembe hasa katika ujumbe unaomuunga mkono mbunge huyo wa zamani wa Kinondoni, huku baadhi wakimpongeza kwa hatua yake.

Mwandishi wetu alipopitia ukurasa huo wa Facebook jana saa 11:30 jioni, wananchi waliokuwa wamejitokeza kumjibu walikuwa wamefikia 63 na wote wakimponda isipokuwa watatu.

Waliompongeza ni Kashinde Kalungwana akisema, “Kwa mujibu wa Katiba watu wako yuko huru kwenda watakako na kuishi popote ilimladi havunji Sheria. Kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni haki yake ya kikatiba.”

Othuman Sefu alimuunga mkono akiandika kuwa wananchi wa Kinondoni watarajie maendeleo maana Mtulia anakwenda kukaa na wapanga bajeti, “Ukiwa mpishi basi watoto wako hawalali njaa.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bunju Cityfc alisema, “Fikra sahihi huja kwa lugha sahihi. CCM ndiyo lugha sahihi kwa fikra sahihi za maendeleo ya Watanzania.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad