PAMOJA na kuachwa katika kikosi cha Simba hivi karibuni, aliyekuwa beki wa timu hiyo, Mzimbabwe, Method Mwanjali, ameisifia klabu hiyo kwa kusema kuwa hajaona kama hiyo katika timu za Afrika alizocheza, kwani ni ya kipekee, huku akiitakia mafanikio mema kwenye michuano yake.
Beki huyu alikuwa nahodha wa kikosi hicho, ameachwa na Simba kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo huku nafasi yake ikichukuliwa na beki Mghana, Asante Kwasi.
Mwanjali alisema kuwa, licha ya kupitia timu kadhaa huko nyuma, Simba ni moja kati ya timu ambazo aliyafurahia maisha alipokuwa akicheza kwa takriban miaka miwili.
“Sina la kusema lakini najua Simba ni klabu kubwa na ya kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na jinsi ambavyo imekuwa ikipambana kuhakikisha inaweka historia katika ramani ya soka pamoja na inavyowatunza wachezaji wake.
“Kila la kheri na mafanikio mema katika michuano yote ambayo ipo mbele yao, wapambane na kuweza kufika mbali zaidi ya walipo sasa,” alisema Mwanjale.
Ikumbukwe kuwa, Mwanjale kwa muda ambao amecheza Simba, amefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la FA pekee msimu uliopita.