Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 70 katika kaunti ya Homa Bay nchini Kenya, amejitoa uhai baada ya kuachwa na mkewe wa pili kwa kumkimbia na kumuachia upweke wa hali ya juu.
Tukio hilo limetokea wiki hii baada ya mke wa mzee huyo Samuel Oloto Onjoga, kutoroka nyumbani katika hali isiyoeleweka na kwenda kuishi katika soko lililo karibu, kitendo kilichomuachia upweke na huzuni.
Chifu wa eneo hilo, Bw Joseph Ndege ameviambia vyombo vya habari kwamba Bw. Onjoga alijitia kitanzi kwa kutumia kamba ya mkonge kwenye mwembe ulioko nyumbani kwake.
"Tulimpata akining’inia kwenye mwembe ulio kando ya nyumba yake, alitumia kamba ya mkonge kujinyonga, mzee huyo alikuwa na upweke baada ya mke wake wa pili kumtoroka na kwenda kukodisha nyumba katika soko lililo karibu baada ya kuzozana,” amesema Chifu huyo.
kwa mujibu wa wanakijiji wenzake mke wa kwanza wa marehemu alifariki miaka mitano iliyopita, na kuoa mke huyo wa pili miaka miwili iliyopita, na kwamba huenda mzee huyo ambaye ni mfanya biashara wa mifugo alipatwa na matatizo ya kimawazo kwa kuishi peke yake nyumbani, ilhali alikuwa pia na matatizo ya kiafya.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Homa Bay, Bw Marius Tum, amesema polisi wameanzisha upelelezi kubainisha ukweli kuhusu kifo hicho, huku mwili wake ukihamishwa katika mochwari ya hospitali ya kaunti ndogo ya Rachuonyo kusubiri kufanyiwa upasuaji wa kubainisha chanzo cha kifo.