Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameusifia wimbo wa Kivuruge ulioimbwa na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Nandy akieleza kuwa umebeba ujumbe mzuri wa masuala yanayotokea kweli katika jamii.
Wimbo huo unamuelezea mwanamke anayelalamikia kusumbuliwa katika mapenzi licha ya kuwa anafanya kila awezalo kumridhisha mpenzi wake.
Kwenye mtandao wa Youtube video ya wimbo huo imetazamwa na watu zaidi ya 600,000, ikiwa ni siku ya nane tangu ilipowekwa kwenye mtandao huo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Dk Tulia ameandika “Kwa jitihada hizi natumaini utafika mbali zaidi, uvumilivu na nidhamu ni vya kuzingatia kwenda kwenye mafanikio. Wimbo wako Kivuruge tumeupokea kwa mikono miwili,”
Mbali na kufuatiliwa zaidi katika mtandao wa youtube, Kivuruge pia imekuwa ikifanya vyema katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni kutokana na kuchezwa mara kwa mara.
Nandy ameingia kwenye orodha ya wasanii wa kike waliofanya kazi kubwa kwenye muziki mwaka 2017 kupitia kazi zake mbalimbali na nyingine alizoshirikishwa.