Kiongozi wa Muungano wa Nasa nchini Kenya, Raila Odinga amesema ataapishwa kuwa rais wa wananchi kama walivyopanga akitaka Rais Uhuru Kenyatta kuacha kumtisha.
Akizungumza alipohudhuria mkutano kujadili kuundwa kwa bunge la wananchi eneo la Pwani, Odinga amesema hakuna atakayemzuia kuapishwa.
“Nitainua Biblia. Hakuna atakayenizuia kuinua Biblia. Ni bora kusimama na ukweli na kufa kwa jambo kuliko kukosa kufanya jambo,” amesema Odinga.
Wiki iliyopita muungano wa Nasa ulitangaza utarejea katika shughuli za kubuni bunge la wananchi baada ya kuahirisha mipango ya kumuapisha Odinga.
Odinga jana alizungumzia suala hilo kwa mara ya kwanza na kutaka Rais Kenyatta kutotoa vitisho kuhusu mipango yake ya kuapishwa.
Amesema hatatishwa na yeyote na kuwa Kenya ni kubwa kuliko yeyote. “Hakuna anayeweza kuja na kuwatisha Wakenya,” amesema.
Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa katika kaunti ya Kilifi, ofisa mkuu mtendaji wa ODM, Oduor Ongwen amesema ratiba ya kumuapisha Odinga katika mkutano wa kitaifa imekamilika.
Hata hivyo, hakutoa tarehe ambayo Odinga ataapishwa. “Tutamuapisha wapende wasipende. Hatutafanya shughuli hiyo kama mzaha, itakuwa katika kongamano la kitaifa na ataanza kutawala mara moja,” amesema Ongwen.