NEC yawashukia CHADEMA kuhusu mgombea Ubunge Singida Kaskazini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeeleza kuwa inawashangaa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaosema kuwa hawamtambui mgombea wa ubunge aliyesimamishwa kugombea katika jimbo la Singida Kaskazini.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhan Kailima ameeleza kuwa CHADEMA kupitia Katibu wa Wilaya wa Singida Vijijini wamekamilisha mchakato wa utambulisho wa mgombea wa Ubunge jimbo la Singida Kaskazini, Joseph Njumbe

“Halmashauri ya Wilaya ya singida wagombea 6 wameteuliwa juzi mmojawapo akiwa bwana Joseph Njumbe wa CHADEAMA. Ameteuliwa kwa sababu amekidhi vigezo vya kikatiba, kisheria na kikanuni yeye na chama chake cha Demokrasia na Maendeleo.”

“Kwa hiyo wanapolalamika kwamba huyu hawamjui nawashangaa sana. Nawashangaa sana kwa saababu Kwa mujibu wa ibara ya 67 ibara ndogo ya 1b ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Mgombea yeyote wa ubunge lazima awe amependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa.”

“Kanuni namba 31 kanuni ndogo ya kwanza ya uchaguzi wa Rais na wabunge ya mwaka 2015, inasema mtu akitaka kugombea ubunge atawasilisha barua yake ya utambulisho iliyosainiwa na katibu wa chama au wa wilaya wa chama husika. Barua yake inawasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi.”

“Huyu Bwana David Joseph Njunbe amewasilisha barua hiyo ya utambulisho iliyosainiwa na katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Singida Vijijini, Bwana Amani M mloya,” amesema Kailima.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Kailima Ramadhani amesema kuwa kwa kupitia kanuni na vigezo vya sheria ya uchaguzi, Mgombea huyo wa CHADEMA amekidhi vigezo vyote vilivyohitajika ili kupitishwa kugombea Ubunge katika jimbo hilo.

Aidha, Kailima ameeleza kuwa Joseph Njumbe, pamoja na kuwa ameshakamilisha taratibu za kupitishwa kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CHADEMA, bado ana haki ya kikatiba ya kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho pale tu atakapotimiza taratibu zinazotakiwa ili kujiondoa.

Kailima aliongeza kuwa Tume ya Uchaguzi haiangalii

“Sisi hatuangalii muhtasari wa kamati kuu ama hatuangalii katiba iliyosajiliwa na Katibu Mkuu wa chama chochote cha siasa. Tunaangalia barua iliyosainiwa na Katibu wa Chama wa Mkoa ama Katibu wa Chama wa Wilaya  na ni kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo,” amesema Kailima.

CHADEMA pamoja na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vilitangaza kutokushiriki uchaguzi huo mdogo wa wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Januari 18, 2018 ikidai kuwa mwenendo wa hali ya kisiasa nchini siyo shwari na kuitaka Tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi huo.

Juzi CHADEMA kupitia Mkuu wake wa Idara ya Mawasiliano, Tumaini Makene ilitoa taarifa kuwa hakijateua mgombea wa ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini na kumtaka Ndugu. Ramadhani Kailima kutambua kwamba mchakato wa uteuzi wa mgombea wa ubunge ndani ya CHADEMA linasimamiwa na Kamati kuu ya Chama hicho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad