Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imejipanga kuanzisha mfuko wa Bima ya Afya kwa watu wote nchini jambo litalosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa kiasi kikubwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile kwenye ziara Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma katika Taasisi ya Kiuma inayomiliki Hospitali, Chuo cha Uuguzi na Kanisa la Upendo wa Kristo.
“Tunatambua kwamba si kila mtu anamudu gharama hizo, kwa bahati mbaya ugonjwa unakuja wakati hatuja jiandaa, serikali imeliona hilo, pamoja na mikakati tunayoendelea nayo ya Bima ya Afya ya NHIF na CHF, tunatarajia kuja na utaratibu wa bima ya afya kwa wote, suala la matibabu lisiwe la kuwaza” alisema Dkt. Faustine Ndugulile.
Dkt. Faustine aliendelea kusema kwamba, Serikali inaendelea kufanya vizuri barani Afrika na Dunia kwa ujumla kwa upande wa utoaji chanjo, kwani imefikia asilimia 97 ya walengwa wote wanaohitaji chanjo nchini jambo linalosaidia kutunza Afya za watu katika jamii.
“Tumefkia hatua kubwa sana ya walengwa wote wanaohitaji kupata chanjo, jambo linaloifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi chache sana zilizofikia malengo hayo” alisema Dkt. Faustine
Aidha Serikali imetoa fedha kwa Vituo vya Afya 172 kwa lengo la kujenga thieta, Chumba cha Kujifungulia, Wodi ya Wazazi, nyumba ya Watumishi na Maabara, Huku Wilaya ya Tunduru ikifanikiwa kupata fedha hizo kwa vituo viwili, kikiwepo kituo cha Afya cha Mkasale.
Kwa upande mwingine Dkt. Faustine ameupongeza uongozi wa Taasisi ya Kiuma kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ikiwemo kutoa huduma za afya kwa wananchi, kutoa ajira, jambo linalotokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Taasisi hiyo hivyo kuipunguzia mzigo Serikali katika nyanja hizo.