YANGA imemuwekea ngumu straika wake Donald Ngoma kwanza kuendelea na kazi yake ya kuitumikia timu hiyo, pia mpango wa kwenda Singida United anakotakiwa na Kocha Hans van Der Pluijm.
Klabu hiyo imesema inamsubiri Kocha wao George Lwandamina arejee kutoka mapumzikoni Zambia, ndipo waamue hatima ya Ngoma aliyepitisha muda alioomba kuwa nje ya timu.
Ngoma hivi karibuni aliaga kwenda kwao Zimbabwe lakini alipitisha muda wa kuwa huo bila kutoa taarifa kwa uongozi, hivyo mabosi wake wanasubiri kukaa kikao cha pamoja na kocha ili kujua hatima yake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Katibu wa Yanga, Charles Mkwasa amesema hawawezi kumtoa Ngoma kumpeleka Singida United kwani bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na timu yao.
“Ngoma bado ni mali yetu na kwa sasa tunataka kukaa naye kuzungumza naye tangu alipoondoka nchini na kwenda kwao Zimbabe kwa ajili ya kupata tiba ya majeraha yake.
“Mshambuliaji huyu bado ana mkataba wa mwaka na nusu hapa hivyo inakua ngumu kumuachia, tunataka amalize mkataba wake uliobakia,” alisema Mkwasa.
Akizungumzia kuhusu hatima ya Ngoma kikosini, Mkwasa alisema; “Inabidi tukae uongozi na kocha ili kujua tunamchukulia hatua gani Ngoma kwani alipitisha muda aliopewa kuwa nje ya timu bila maelezo, tutasikiliza kile anachosema sasa na tutapima kuhusu hatua za kumchukulia.”
Ngoma Akwaa Kisiki Yanga Hatima Yake Ipo Mikononi mwa Lwandamina
0
December 02, 2017
Tags