Omog Amtengenezea Mazingira ya Kubaki Simba Mavugo

Omog Amtengenezea Mazingira  ya Kubaki Simba Mavugo
WAKATI habari zikizagaa kwamba Simba ipo mbioni kuachana na straika wake, Laudit Mavugo, Kocha Joseph Omog wa timu hiyo ameenda mapumziko kwao Cameroon akisisitiza mchezaji huyo asiachwe ili kuepuka gharama za kuvunja mkataba wake.

Omog tayari yupo Cameroon tangu Jumatano ya wiki hii, inaelezwa ameacha ripoti kwa uongozi wa Simba inayowasisitiza kuliacha jina la Mavugo raia wa Burundi katika kikosi chake.

Mavugo hadi sasa amefunga mabao mawili tu katika Ligi Kuu Bara ambapo Simba ina mabao 23, hivyo uwezekano wa kuachwa ulikuwa mkubwa akiwa amejiunga na timu hiyo msimu uliopita akitoka Vital’O ya kwao Burundi.

Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Omog ameamua kumbakisha Mavugo kikosini si kwa sababu ya uwezo bali anataka amalize mkataba wake miezi sita ijayo ili awe huru kuondoka.

“Kweli kulikuwa na mipango hiyo ya Mavugo kuachwa lakini kwa sasa suala hilo limesitishwa kwa sababu Omog amependekeza asiachwe katika kipindi hiki bali hadi pale mkataba wake utakapomalizika.

“Kocha ameona afanye hivyo kwa sababu ya kutopoteza fedha za kulipa gharama za kuvunja mkataba maana anaweza kukataa kwenda kwa mkopo popote pale, tutabaki naye ili baadaye aondoke kwa amani,” alisema bosi huyo.

Habari kutoka Yanga zilisema, klabu hiyo ilikuwa ikimpigia hesabu Mavugo endapo angeachwa na Simba imuwahi kumsajili ikiamini bado ana makali isipokuwa hapati nafasi katika timu yake.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad