Papa Francis Awatea Wahamiaji

Papa Francis   Awatea Wahamiaji
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewataka Wakristo bilioni 1.3 duniani kutopuuza majanga yanayowakumba mara kwa mara wahamiaji “wanaofukuzwa kutoka nchi zao” na viongozi ambao wako tayari “kumwaga damu kwa watu wasio kuwa na hatia”.

Pia, kiongozi huyo amewataka waumini hao kuwa wakarimu na watu wenye huruma kwa wahamiaji. Amesema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika Sikukuu ya Krismasi.

Papa Francis, ambaye anajulikana kwa jina lake aliopewa na wazazi wake Jorge Bergoglio, mjukuu wa wahamiaji kutoka Italia, alizungumzia kuhusu hatima ya wakimbizi miaka mitano baada ya kuchukua uongozi wa Kanisa Katoliki duniani.

“Hakuna mtu anayepaswa kuhisi kuwa hana mahali hapa duniani,” alisema katika hotuba yake ya Krismasi.

Hayo yanajiri wakati ambapo kumeendelea kushuhudiwa makabiliano kati ya waandamanaji wa Kipalestina na wanajeshi wa Israel huku Wapalestina 12 wakipoteza maisha.

Uamuzi wa Marekani kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel umeelezwa na washirika wa Palestina kuwa umehatarisha uwezekano wa kupatikana kwa amani kati yake na Israel.

Kadhalika kiongozi huyo amewaombea watu wa kisiwa cha Mindanao nchini Ufilipino.

Kisiwa hicho kimeharibiwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi baada ya kukumbwa na kimbunga tokea siku ya Ijumaa.

Papa Francis amesema dhoruba hiyo imewaathiri watu wengi na imesababisha uharibifu mkubwa. Papa Francis amesema anataka kuwahakikishia watu wa Mindanao sala zake ambapo alimuomba Mungu mwenye huruma apokee roho za waliokufa kwenye maafa hayo na wakati huo huo amewafariji wote wanaohusika waliofikwa na misiba. Zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha kutokana na dhoruba hiyo huku wengine zaidi ya 140 wakiwa hawajulikani waliko.

Mjini Bethlehem nchini Israel, mji ambao Wakristo wanaamini kuwa Yesu alizaliwa, mwaka huu shamrashamra zinashuhudiwa lakini si kwa kiasi kikubwa.

Wasiwasi unashuhudiwa na watalii wengi, hawajakwenda katika mji huo kwa kuhofia usalama wao.

Hatua hii inakuja baada ya Marekani hivi karibuni, kutambua mji wa Jerusalem kama makao makuu ya Israel hatua ambayo imeikasirisha Palestina na mataifa ya Kiislamu na yale ya Kiarabu.

Wiki iliyopita kulikuwa na mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa kulaani hatua hiyo ya Marekani. Katika hatua nyingine, waamini wa Kanisa Katoliki waliobahatika kupata nafasi katika maisha ya kisiasa wameaswa kuhakikisha wanasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Wakati huohuo, ujumbe wa Vatican umewataka wanachama wa Umoja wa Mataifa daima kuzingatia historia na utambulisho maalum wa mji wa Yerusalemu ambao kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa.

Jerusalemu ni mji mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Ujumbe wa Vatican umesema kuwa suluhu ya amani katika eneo hilo itafikiwa kwa kuheshimu.

“Jumuiya ya kimataifa inaweza kusaidia kukuza na kudumisha misingi kuwepo kwa amani na hivyo kuuwezesha mji wa Jerusalemu kutunza umaarufu wake katika mchakato wa majadiliano na upatanisho,” umesema.

Ujumbe huo umewashuruku wanachama wa Umoja wa Mataifa, kwa kusimama kidete kulinda maamuzi ya UN ambayo imesaidia kudhibiti ghasia na machafuko ambayo yangeweza kujitokeza katika eneo hilo baada ya kupitisha azimio la kulaani hatua ya Marekani kuutambua mji wa Jerusalemu kama makao makuu ya Israel

Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuzingatia maana ya Sikukuu ya Krismasi kwa kuzingatia utu na matendo mema na kuacha kuendekeza mwelekeo wa sasa ambao umegeuza sikukuu hiyo kuwa ni tukio la kibiashara na ulaji wa kupindukia.

Kardinali Parolin, amewataka wanasiasa kutumia vyema dhamana na wajibu wao, kwa kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa kero na mahangaiko ya wanawanchi wa kawaida.

“Inasikitisha kuona siasa inageuzwa kuwa ni jukwaa la uchu wa mali, madaraka na mafao ya mtu binafsi, kiasi cha kusahau na kufumbia macho mahangaiko, matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wanao wawakilisha.

Siasa imekuwa ni uwanja wa malumbano, kejeli na vijembe mambo yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi,” alisema.

Alisema baadhi ya wanasiasa wamegeuka wajeuri na watu wenye kiburi kiasi cha kutupilia mbali fadhila ya unyenyekevu inayowasogeza zaidi kwa wananchi wa kawaida.

Alisema wanasiasa wanapaswa kutumia jukwaa la kisiasa kama uwanja wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad