Kiongozi wa upinzani nchini Kenya kupitia NASA, Raila Omolo Odinga, amesema yupo tayari kufa ikiwa ndiyo gharama atakayolipa baada ya kuapishwa kama rais wa wananchi, lakini lazima haki itendeke.
Raila Odinga ametoa kauli hiyo alipokuwa kwenye mazishi ya Mbunge wa nchi hiyo Francis Nyenze katika eneo la Kitui, na kueleza kwamba ataapishwa kuwa rais hata kama itamgharimu hukumu ya kifo kwa kufanya hivyo.
"Iwapo kifo ndio gharama ambayo lazima tuilipe kwa haki ya uchaguzi Kenya, na kwamba hakutakuwa na dhuluma za uchaguzi tena baadaye, tupo tayari kulipa hiyo gharama, tutaapishwa na wafanye kile wanataka kufanya", alisikika Raila Odinga.
Odinga aliendelea kwa kusema kwamba alishinda uchaguzi wa Agosti 2017 ambao ulifutwa na Mahakama ya Juu, na kuapa kuendelea kupambana kuleta mabadiliko katika uongozi wa nchi.
"Tulisema tulishindauchaguzi na tutaapishwa, tumeonywa kwa hukumu na kifo, nataka nimwambie Githu Muigai (Mwanasheria Mkuu wa Kenya) na bosi wake, tutaapishwa na tutaufa", amesema Odinga.
Hivi karibuni Mwanasheri aMKuu wa Kenya amemuonya Raila Odinga kuendelea na mpango wake wa kujiapisha wakati tayari kuna Rais aliyeapishwa kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, na kusema kwamba sheria itachukua mkondo wake.