Serikali Kuzifutia Leseni Kampuni 12 za Madini

Serikali Kuzifutia Leseni Kampuni 12 za Madini
Serikali imewashukia wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambao hawalipi kodi na imelenga kufuta leseni zote kwenye migodi hiyo isiyolipa kodi Serikalini.

Hadi hivi sasa kampuni  12 za wachimbaji hao wa madini ya Tanzanite, zinadaiwa  zaidi ya Sh3bilioni na zitakazoshindwa kulipa kodi hiyo zitafutiwa  leseni zao na wizara ya madini.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amesema leo Desemba 22  mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, wakati akizungumza na wafanyabiashara na wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite.

Mnyeti alisema Serikali haiwezi kung'ang'ania kampuni moja ya TanzaniteOne pekee kwenye kuingiza kodi ili hali zipo kampuni nyingine ambazo hazilipi kodi kwa kisingizio cha kutozalisha madini hayo .

Alisema wachimbaji hao wanamiliki kampuni za uchimbaji na wanachimba kwa teknolojia kama kampuni ya TanzaniteOne lakini hawalipi chochote serikalini.

"Serikali inanyonya kwenye TanzaniteOne kuingiza mapato hawa wengine hawalipi kodi, sasa ni lazima tukubaliane madeni hayo yanalipwaje na watakaoshindwa watafutiwa leseni, zao," alisema Mnyeti.

Alisema kampuni itakayoshindwa kulipa kodi itapisha eneo hilo kwani miaka yote wanachimba hawalipi kodi ya serikali na mapato yote wanaondoka nayo kwa kisingizio kuwa hawajapata chochote.

"Tuliunda tume ya kuchunguza hizi kampuni na tukabaini hazilipi  kodi, sasa sisi serikali tukishindwa kusimamia kodi ili wananchi wapate maendeleo ni bora tukalale nyumbani na kulima viazi kuliko kushindwa kukusanya kodi," amesema  Mnyeti na kuongeza.'

"Mapato yote wanayopata wanaondoka nao na serikali haipati chochote ukimuuliza eti hajawahi kupata sasa kama haujapata ni bora uondoke , kamishna wa madini nadhani unanisikia vizuri, nitakuletea majina ya wanaoshindwa kulipa kodi ufute leseni zao," amesema

Hata hivyo, alisema madini ya Tanzanite yanapaswa kuwa baraka na siyo laana hivyo yanatakiwa kutumika kwa ajili ya kuwatetea maendeleo ya watanzania na kuleta tija kwa Taifa.

Naibu Waziri wa Madini Ladslaus Nyongo amesema  wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuona wajibu wa kufuata sheria za nchi ikiwemo kulipa kodi za serikali na mrabaha kwa uhuru na uwazi kabisa.

Nyongo amesema  serikali imelenga kufanya mji mdogo wa Mirerani kuwa kitovu cha biashara ya Tanzanite duniani.

Alisema wadau wa madini wanapaswa kuwekeza kwenye huduma muhimu kama vile hoteli za kisasa, mabenki, maduka ya kisasa na huduma nyingine.

Mkurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne, Hussein Gonga amesema anashukuru uamuzi wa Rais John Magufuli kuagiza mnada wa madini kufanyika eneo linalochimbwa madini hayo.

Gonga amesema  jamii inayozunguka eneo hilo imenufaika kupitia mnada huo kwa kufanya biashara mbalimbali kwa wadau wa madini ikiwemo nyumba za kulala wageni, vyakula, vinywaji na mengineyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad