Shomari Kapombe ni ‘kipaji kilichopotea’ au ‘kujipoteza?’


Na Baraka Mbolembole

ILIONEKANA kama vile Shomari Kapombe angekuwa mwanasoka wa kwanza raia wa Tanzania kucheza soka katika ligi ya juu nchini Ufaransa wakati mlinzi huyo wa kulia aliposajiliwa na AS Cannes mwaka 2013 akiwa U23.

Sikuwahi kuwa na shaka kuhusu ubora wa kujituma, kiuchezaji na tamaa ya mafanikio alivyonavyo mlinzi huyo wa klabu ya Simba ambaye ni kati ya vijana waliopata bahati ya kuruka kutoka Moro Youth Soccer Academy hadi kusajiliwa na kucheza ligi kuu Tanzania Bara mwaka 2011 akiwa mchezaji wa timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania U23.

Kapombe hakuchelewa kuingia katika beki ya kati pale Simba wakati huo kukiwepo pia wazoefu kama Victor Costa, Juma Nyosso, Kelvin Yondani. Alikuwa chaguo la kwanza chini ya kocha Moses Basena na baadae Milovan Cirkovic na akatokea kuwa beki bora wa pembeni nchini huku akihodhi namba mbili ya Taifa Stars.

Msimu wake wa kwanza Simba uliambatana na ubingwa Mei, 2012 huku akiwemo katika kikosi kilichowateketeza mahasimu wao Yanga 5-0 na kufika hatua ya ‘play off’ katika Caf Confederation Cup 2012. Uwezo wake wa kupandisha mashambulizi na kutengeneza magoli kwa wachezaji wenzake huku akifunga mara kadhaa ulimfanya atabiriwe na wengi kufika mbali kimpira.

Lakini miaka mitano sasa ni ‘aibu’ kwa mchezaji huyo kushinda taji moja tu la ligi, huku pia ndani ya uwanja akiwa mbali na tarajio la wengi kumuona akicheza nje ya Tanzania.

Kwanini alirudi Tanzania?

Novemba 2013 alipokuja kuichezea Tanzania, Kapombe hakutaka tena kurejea Ufaransa katika klabu yake ya Cannes na sababu kubwa aliyotoa ni klabu hiyo kushindwa kumlipa mshahara wake (inasemekana ni wa mwezi mmoja tu) Kapombe aliendelea kubaki nchini huku akijifua binafsi. Baadae akashinikiza kuuzwa na klabu hiyo iliona hakuna namna ikakubali kumuuza Azam FC katikati ya mwaka 2014.

Kuna mambo mengi yalimvutia Kapombe kuondoka Ufaransa na kurejea nchini. Inasemekana Azam FC ilikubali kuwaajiri ndugu wasiopungua watano wa Kapombe, Si hivyo tu mchezaji huyo na ndugu zake waliahidiwa kupelekwa na kugharimiwa matibabu mahala kokote pale kama ingetokea ulazima wa mgonjwa kufanyiwa hivyo, pia mchezaji mwenyewe aliahidiwa mshahara ambao hakuwahi kuupata Simba wala Cannes. Hadi anaumia katikati ya mwaka huu wakati akiichezea TaifaStars, Kapombe alikuwa mlinzi bora namba mbili nchini, ila si kwa kiwango kile ambacho kilimfanya Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ kuwashinikiza Simba kumsaini kijana huyo akiwa na miaka 19 mwaka 2011.

Matatizo ya kiafya na majeraha yasiyokwisha kwa kiasi kikubwa yamemrudisha nyuma mlinzi huyo bora lakini kwa namna nyingine yeye mwenyewe pia anapaswa kujilaumu kwa hatua yake ya kuondoka Ufaransa wakati angali kinda kwa sababu za kimaslahi. Kapombe aliamini ni bora kucheza Tanzania kuliko daraja la nne Ufaransa lakini kwa miaka hii minne angekuwa wapi kama angeamua kukaza kama Mbwana Samatta ambaye alianza na mshahara mdogo TP Mazembe ambako alidumu kwa misimu mitano na sasa ni staa wa KRC Genk katika ligi kuu ya Ubelgiji huku akipata kipato cha juu zaidi ya kile alichokuwa akipewa TP?

Anaweza kutamba kwa mara nyingine na kufikia ndoto zake

Mlinzi huyo anatarajiwa kuanza kuonekana kwa mara ya kwanza akiichezea Simba tangu alipokubali kurejea klabuni hapo Agosti mwaka huu akitokea Azam FC. Licha ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara tangu alipokuwa Azam FC, Kapombe ni mchezaji ambaye hujituma na kuonyesha kiwango cha juu kila anapokuwa uwanjani.

Jambo la muhimu kwake hivi sasa ni kucheza kwa tahadhari, huku ikisemwa kuwa mchezaji huyo amekuwa muoga tangu alipopata matatizo ya tumbo miaka miwili iliyopita ni wazi itakuwa vigumu sana kwake kurejea katika ubora ambao watazamaji wamezoea kuuona anapokuwa uwanjani.

Bado ni kijana mdogo na kama Simba watamuhudumia kama walivyokuwa wakifanya Azam FC watamsaidia kurudisha ubora wake lakini wakimsema vibaya kama alivyofanya Zacharia Hans Poppe basi mwisho wa mchezaji huyo kuonekana katika jezi za klabu kubwa nchini itakuwa Mei, 2018 na huko kwingineko atakapokwenda ni wazi itakuwa ni kuhitimisha tarajio kubwa la watanzania ambao waliamini kijana huyo angecheza mahala kokote pale nje ya Tanzania.

Kwa kweli Kapombe yuko mbali sana na kiwango chake kilichomfanya wengi wamtabirie makubwa, ila bado anaweza kujaribu kupambana wakati nafasi yake ya mwisho itakaporejea Simba. Alishafanya makosa kurudi Tanzania mahala ambako mchezaji ‘majeruhi hathaminiwi’ hata kidogo.

Naamini hiki ni kipaji bora ambacho kimepotea kwa sababu kilitaka kupotea chenyewe. Kuondoka Simba hadi Cannes mwaka 2013 utabaki kuwa uamuzi bora kuwahi kufanywa na mchezaji huyo. Kulazimisha kuondoka Cannes na kujiunga Azam FC mwaka 2014 ilikuwa ni uamuzi mbaya japo kuna watu wake waliweza kunufaika. Kuondoka Azam FC na kurejea Simba kwa mara ya pili Agosti, 2017 ni uamuzi mbaya zaidi kuwahi kufanywa na Kapombe, wapi sasa atakwenda? Hakika hiki ni kipaji kinachokwenda kupotea tena kikiwa kimecheza VPL kwa misimu sita tu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad